2016-03-14 09:57:00

Papa Francisko na mapambazuko ya utumishi wake!


Baba Mtakatifu Francisko ameanza maadhimisho ya mwaka wake wa nne kama Khalifa wa Mtakatifu Petro kwa kuchapisha Waraka wa Kitume kuhusu familia. Haya ni matunda ya maadhimisho ya Sinodi mbili za Maaskofu kuhusu familia zilizoadhimishwa hapa mjini Vatican kwa kipindi cha miaka miwili. Wito na utume wa Familia katika Kanisa na Ulimwengu mamboleo, ndiyo kauli mbiu iliyoongoza maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya familia mwezi Oktoba 2015. Huu ni Waraka wake wa tatu baada ya kuchapisha kwanza kabisa “Evangelii gaudium” Injili ya furaha, kuhusu umuhimu wa kutangaza na kushuhudia Injili ya furaha kwa watu wa nyakati hizi ambazo wanaonekana kukata na kukatishwa tamaa na changamoto mbali mbali wanazokumbana nazo katika ulimwengu mamboleo!

Waraka wa pili ni “Laudato si” “Sifa iwe kwako” juu ya utunzaji wa nyumba ya wote. Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka huu anapembua kwa kina na mapana jinsi ambavyo uharibifu wa mazingira unavyopaswa kujikita katika toba na wongofu wa ndani katika ekolojia, ili kuwa na mageuzi makubwa katika maisha na kuwajibika katika utunzaji bora wa mazingira, nyumba ya wote. Hii ni dhamana ya kijamii inayopania pamoja na mambo mengine, kung’oa umaskini, kwa kuwajali na kuwathamini maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii, ili kweli rasilimali ya dunia iweze kutumika vyema kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya wengi; furaha, haki, amani na utulivu!

Baba Mtakatifu Francisko tangu kuchaguliwa kwake ameendelea kutoa kipaumbele cha kwanza kwa ajili ya Injili ya Kristo inayopaswa kutangazwa na kushuhudiwa katika uhalisia wa maisha, kielelezo cha imani tendaji. Kwa namna ya pekee kabisa, Baba Mtakatifu ameguswa na mahangaiko, matatizo na changamoto wanazokumbana nazo wanafamilia sehemu mbali mbali duniani. Kuna wanawake na wanaume wanaoendelea kusimama kidete kulinda na kudumisha tunu msingi za maisha ya ndoa na familia; katika magonjwa na umaskini; katika raha na shida!

Baba Mtakatifu anakaza kusema, familia zinapaswa kulindwa, kutunzwa na kudumishwa; kwa kuonesha mshikamano wa upendo na familia zinazokabiliana na changamoto za maisha. Hapa dhana ya Sinodi katika maisha na utume wa Kanisa imepewa dhamana ya pekee kama jukwaa la majadiliano kati ya familia ya Mungu, ili kukuza na kudumisha pia majadiliano ya kidini na kiekumene kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya familia ya binadamu katika ujumla wake.

Baba Mtakatifu Francisko anaendelea na utekelezaji wa mageuzi ndani ya Kanisa, mambo yanayohitaji kwa namna ya pekee toba na wongofu wa ndani. Anatambua kabisa kwamba, mchakato huu si rahisi sana kukubaliwa na kupokelewa, daima utapambana na vikwazo na kinzani, lakini ni muhimu sana katika maisha na utume wa Kanisa. Waamini watambue na kukumbuka kwamba, huruma ni kiini na muhtasari wa imani ya Kikristo. Kumbe, maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu ni muda uliokubalika wa toba na wongofu wa ndani, ili kuambata huruma na upendo wa Mungu, tayari kumwilisha Injili ya huruma ya Mungu katika uhalisia wa maisha ya watu!

Wakati huo huo, Kardinali Agostino Vallini kwa niaba ya Familia ya Mungu Jimbo kuu la Roma, anamtakia heri na baraka Baba Mtakatifu Francisko anapoanza mwaka wake wa nne kama Khalifa wa Mtakatifu Petro. Katika changamoto zinazoendelea kujitokeza ndani ya Kanisa na katika ulimwengu mamboleo, Baba Mtakatifu Francisko bado ni rejea katika masuala ya kiroho na kimaadili. Familia ya Mungu sehemu mbali mbali za dunia inatambua na kuthamini mchango wake katika medani mbali mbali za maisha ya binadamu! Ushuhuda wa maisha yake ni mwanga angavu kwa Kanisa na walimwengu! Waamini kutoka sehemu mbali mbali za dunia waliokuwa kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, Jumapili tarehe 13 Machi 2016 wamemtakia heri na baraka, ujasiri na mafakio mema katika maisha na utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro, wao wanaendelea kumsindikiza kwa njia ya sala!

Na vijana wanaohudumiwa na Kituo cha Mshikamano wa Kitaifa nchini Italia kilichoanzishwa na Padre Mario Picchi, ambacho hivi karibuni, kilibahatika kutembelewa na Baba Mtakatifu Francisko kama sehemu ya utekelezaji wa matendo ya huruma Ijumaa ya huruma ya Mungu, wanamwombea ili aendelee kuwa ni shuhuda na chombo cha kuhamasisha haki, amani, ustawi na maendeleo ya wengi. Baba Mtakatifu aendelee pia kuwaimarisha ndugu zake katika imani, matumaini na mapendo!

Jumuiya ya Mtakatifu Egidio yenye Makao yake makuu mjini Roma, inampongeza Baba Mtakatifu Francisko kwa kujenga na kuendelea kuimarisha mchakato wa ujenzi wa madaraja ya watu kukutana katika medani mbali mbali za maisha, ili kuvunjilia mbali kuta za ubaguzi na utengano kati ya watu. Huu ndio mwelekeo wa Baba Mtakatifu Francisko katika diplomasia ya kimataifa na cheche za mafanikio zinaanza kuonekana taratibu huko Cuba na Marekani; Kati ya Kanisa Katoliki na Kanisa la Kiorthodox la Moscow na Russia nzima, bila kuisahau Familia ya Mungu Afrika ya Kati, mahali alipofungua Lango la Huruma ya Mungu kwa ajili ya maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.