2016-03-14 07:03:00

Onesho la Jubilei!


Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican kwa kushirikiana na Bwana Pietro Grasso, Rais wa Senate ya Italia, tarehe 15 Machi 2016 watazindua Onesho la historia ya maadhimisho ya Jubilei yanayoongozwa na kauli mbiu “Antiquorum habet”. Onesho hili litafanyika kwenye Ukumbi wa Zuccari, Jengo la Giustiniani na litadumu hadi Mei, Mosi, 2016.

Taarifa zinaonesha kwamba, maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu na kumbu kumbu ya miaka mitatu tangu Baba Mtakatifu Francisko alipochaguliwa kuliongoza Kanisa Katoliki kama Khalifa wa Mtakatifu Petro ni nafasi nzuri kwa majujaji na wageni kufanya tafakari ya kina kuhusiana na historia ya maadhimisho ya Jubilei kuanzia mwaka 1300 hadi nyakati hizi! Hapa mambo msi haba!

Mahujaji na wageni wataweza kushuhudia nyaraka na picha mbali mbali zilizopigwa nyakati hizo ambazo kwa sasa zimehifadhiwa na Ofisi ya Senate ya Italia. Onesho hili litatajirishwa kwa namna ya pekee na baadhi ya nyaraka na picha kutoka kwenye Makumbusho ya Vatican na Maktaba ya Kitume ya Vatican. Onesho hili linajikita kwa namna ya pekee katika maadhimisho ya Jubilei kwa kuonesha mwelekeo wa kijamii na maisha ya hadhara, yanayowashirikisha wengi. Kiini cha onesho hili ni hujaji, maeneo ya hija yaliyoko mjini Roma sanjari na kuonesha mabadiliko na mambo yanayounganisha Roma na historia ya maadhimisho ya Jubilei.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.