2016-03-14 06:41:00

Hata mimi sikuhukumu! Nenda zako usitende dhambi tena!


Baba Mtakatifu Francisko katika tafakari yake wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana, Jumapili tarehe 13 Machi 2016 amefafanua kwa kina Injili ya Jumapili ya tano ya Kwaresima ambayo Yesu aliletewa mwanamke aliyefumaniwa katika uzinzi ili aweze kumtolea hukumu ya kifo! Kufumba na kufumbua mwanamke akajikuta yuko mbele ya Yesu, huku akiwa amezungukwa na umati mkubwa; alikuwa kati kati ya huruma ya Mungu na adhabu ya kifo pamoja na hasira ya washitaki wake. Hawa ni watu ambao walitaka kumjaribu Yesu na wala hawakuwa na nia njema ya kutaka kujifunza kutoka kwa Yesu, Bwana na Mwalimu.

Ikiwa kama Yesu angeridhia adhabu ya kifo, angepoteza heshima yake ya kuwa ni mpole, mwema na mwenye huruma; ili aweze kuambata utambulisho wake, ilimbidi Yesu kwenda kinyume cha matarajio ya wale watu na kinyume cha Sheria ambayo Kristo mwenyewe aliwahi kusema kwamba, amekuja kuitekeleza! Yesu alipoulizwa kuhusu msimamo wake, hakutoa jibu la mkato, huo ukawa ni mwaliko kwa watu kutuliza ghadhabu zao, ili kutenda kwa haki mintarafu haki ya Mungu. Lakini wale watu walizidi kumsonga Yesu kwa maswali wakitaka atoe maamuzi, huku wakiwa tayari na mawe mikononi mwao, kumshughulikia yule mwanamke mzinzi.

Lakini Yesu akawaambia, yule asiyekuwa na dhambi, awe ni mtu wa kwanza kumtwanga kwa mawe! Lakini wale watu walipochunguza dhamiri zao, kila mtu akaondoka kimya kimya wakianzia wale wakuu hadi wale wadogo. Baba Mtakatifu anakaza kusema, ni vyema kila mtu kutambua kwamba, ni mdhambi na anahitaji huruma na msamaha kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Inapendeza ikiwa kama waamini watakuwa na ujasiri wa kuweka chini mawe yao, tayari kuchunguza dhamiri zao, ili kutambua cheche za dhambi zilizoko ndani mwao.

Baba Mtakatifu anakaza kusema, yule mwanamke akajikuta akiwa amebaki peke yake na Yesu; udhaifu wa mwanadamu na huruma ya Mungu. Hivi ndivyo inavyotokea wakati mwamini anapojikuta mbele ya kiti cha maungamo; anapogundua udhaifu wake wa kibinadamu, tayari kuomba na kuambata huruma ya Mungu. Yesu akamuuliza yule mwanamke! Je, washitaki wako wa wepi? Yesu akamwonesha yule mwanamke mzinzi uso wa huruma na upendo wa Mungu kiasi cha kugundua tena ndani mwake utu uliochafuliwa na dhambi, lakini bado alikuwa na nafasi ya kuweza kufanya mabadiliko kwa kutoka katika utumwa wa dhambi na kuanza kutembea katika njia mpya!

Baba Mtakatifu anakaza kusema, kila mtu ni mdhambi mbele ya Mwenyezi Mungu kwani amesaliti uaminifu wake. Anawakumbusha wengi kwamba, Mwenyezi Mungu kamwe hafurahii kifo cha mdhambi, bali aweze kutubu na kuokoka. Yesu ni chemchemi ya neema inayomwokoa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na kifo. Yesu alipoandika ardhini anawakumbusha wanadamu wote kwamba wao wamumbwa kutoka mavumbini! Mwenyezi Mungu kamwe hapendi kumpatiliza mdhambi kutokana na dhambi zake; hamtambui mtu kutokana na dhambi alizotenda. Mwenyezi Mungu anataka kuwaokoa waja wake, changamoto kwa waamini pia kutamani jambo hili jema; kwa kutubu na kuongoka ili kutenda mema na kwamba, jambo hili linawezekana kwa neema na baraka kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Bikira Maria awasaidie waamini kujiaminisha kwa huruma ya Mungu, ili kweli kuweza kuwa ni viumbe wapya!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.