2016-03-12 08:27:00

Ziara ya Askofu Mkuu Gallagher nchini Uingereza!


Askofu mkuu Paul Richard Gallagher, Katibu mkuu wa mambo ya nchi za nje na ushirikiano wa kimataifa mjini Vatican, hivi karibuni amehitimisha ziara ya kikazi nchini Uingereza ambako amepata nafasi ya kukutana na kuzungumza na viongozi wa Kanisa na Serikali ya Uingereza. Kati ya mambo yaliyopewa kipaumbele cha pekee ni: mchakato wa majadiliano ya kiekumene na ushirikiano kati ya Wakristo kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya wengi; wakimbizi na wahamiaji; athari za mabadiliko ya tabianchi katika nchi wanachama wa Jumuiya ya Madola!

Askofu mkuu Paul Richard Gallagher wakati wa ziara yake ya kikazi nchini Uingereza ameandamana na Askofu mkuu Antonio Mennini, Balozi wa Vatican nchini Uingereza. Amekutana na kuzungumza na Askofu mkuu Justin Welby, kiongozi mkuu wa Jumuiya ya Waanglikani duniani. Wamefurahishwa na uhusiano mwema uliopo kati ya Makanisa haya mawili huko nchini Uingereza na kwamba, kuna haja ya kuendeleza majadiliano ya kiekumene, ili kumshuhudia Kristo na Kanisa lake, kielelezo cha imani tendaji!

Changamoto ya wakimbizi na wahamiaji na umuhimu wa kulinda na kudumisha haki zao msingi kama binadamu. Ni kati ya mada zinazoendelea kupewa kipaumbele cha pekee na Jumuiya ya Kimataifa. Hii ni mada ambayo imejadiliwa kati ya Askofu mkuu Gallagher na Bibi Theresa May, Waziri wa mambo ya ndani nchini Uingereza. Wamegusia umuhimu wa kuwalinda watoto katika matumizi ya mitandao ya kijamii pamoja na viongozi hawa kutambua mchango wa Kanisa Katoliki nchini Uingereza. Akizungumza na Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Uingereza anayeshughulikia masuala ya kimataifa Bwana David Lidington, wamegusia masuala yanayohitaji kupewa msukumo wa pekee ili kulinda na kutetea utu na heshima ya binadamu.

“Sifa iwe kwako, juu ya utunzaji bora wa mazingira”, Laudato si ni waraka ambao unaendelea kupewa kipaumbele cha pekee kama sehemu ya mchakato wa kukabiliana na changamoto za athari ya mabadiliko ya tabianchi sehemu mbali mbali za dunia! Masuala ya kitaifa, kikanda na kimataifa yamejadiliwa na kupewa msukumo wa pekee wakati wa ziara hii ya kikazi huko Uingereza. Athari za mabadiliko ya tabianchi katika mataifa wanachama wa Jumuiya ya Madola; ustawi, maendeleo na mafao ya wengi; Sera za mambo ya nchi za nje zinazopewa kipaumbele cha pekee katika uongozi wa Baba Mtakatifu Francisko kwa sasa!

Askofu mkuu Gallagher wakati wa ziara yake amegusia pia umuhimu wa dini katika Jumuiya ya Kimataifa. Amejibu maswali yaliyoulizwa na wafanyakazi wa Jumuiya ya Madola na Wizara ya mambo ya nchi za nje na ushirikiano wa kimataifa nchini Uingereza. Askofu mkuu Gallagher amekazia umuhimu wa kuendeleza majadiliano ya kidini kati ya waamini wa dini mbali mbali, ili kufahamiana na kushirikiana, ili kwa pamoja, dini ziweze kuwa mstari wa mbele katika kukuza na kudumisha ustawi, maendeleo na mafao ya wengi! Waamini wajenge madaraja ya watu kukutana na kusaidiana; ili kwa pamoja waweze kuwa kweli ni mashuhuda na vyombo vya haki, amani na mshikamano. Hapa kuna haja pia ya kudumisha majadiliano ya kiekumene, ili kuwa na utambulisho na utume wa dini katika maisha na vipaumbele vya watu.

Askofu mkuu Gallagher amefafanua kwa kina na mapana Nyaraka za Baba Mtakatifu Francisko kuhusu utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote na Injili ya furaha, alipokutana na wafanyakazi wa Kituo cha “Royal United Services Institute”. Amegusia pia nafasi na dhamana ya Baba Mtakatifu Francisko katika maisha na utume wa Kanisa pamoja na upendeleo wake wa pekee kwa maskini, utunzaji bora wa mazingira; wakimbizi na wahamiaji pamoja na waathirika wa utamaduni wa utandawazi usiojali wala kuguswa na mahangaiko ya wengine.

Baba Mtakatifu Francisko anajitambulisha kuwa ni kiongozi wa kiroho mwenye dhamana ya kimaadili pia kwa Jumuiya ya Kimataifa. Ni kiongozi anayezungumza, kutenda na kusimamia maamuzi yake. Kwa hakika anapenda kuona Jumuiya ya Kimataifa ikiwa na mwelekeo mpya katika masuala mbali mbali ili kuvuka vikwazo na kinzani ambazo zilisababisha vita baridi; mipasuko ya kidini na kijamii, ili kuanza upya mchakato wa ujenzi wa madaraja ya watu kukutana na kusaidiana. Hapa kipambele cha pekee ni utu na heshima ya binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu.

Baba Mtakatifu Francisko tangu mwanzo wa uongozi wake, miaka mitatu iliyopita, amejielekeza zaidi na zaidi kama mjumbe wa amani na upatanisho huko Mashariki ya Kati na Amerika. Matokeo yake ni Cuba pamoja na Marekani kurejesha tena mahusiano ya kidiplomasia baada ya nchi hizi mbili kusigana kwa takribani miaka hamsini, lakini walioteseka zaidi ni wananchi wa kawaida. Utume huu wa Baba Mtakatifu anakaza kusema Askofu mkuu Gallagher unapata chimbuko lake katika Injili inayowahamasisha watu kujenga umoja, udugu na upendo; ili kuimarisha misingi ya haki, amani na maridhiano kati ya watu! Ziara ya Askofu mkuu Paul Richard Gallagher imekuwa na mafanikio makubwa huko nchini Uingereza kutokana na ushirikiano na Baraza la Maaskofu Katoliki Uingereza na Walles, Ubalozi wa Vatican nchini Uingereza pamoja na Serikali ya Uingereza katika ujumla wake!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.