2016-03-12 07:17:00

Papa na wasaidizi wake washuka kutoka Jangwani!


Baba Mtakatifu Francisko pamoja na wasaidizi wake wa karibu, Ijumaa tarehe 11 Machi 2016 wamehitimisha safari yao “Jangwani”, kipindi cha Juma zima lililotawaliwa na: Ukimya, sala, tafakari, Ibada ya Kuabudu Ekaristi Takatifu pamoja na maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu, chanzo na kilele cha maisha na utume wa Kanisa. Katika shukrani zake kwa Padre Ermes Ronchi aliyepewa dhamana na wajibu wa kumwongoza Baba Mtakatifu na wasaidizi wake katika tafakari ya Kwaresima ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu, amesema kuna haja ya kugundua tena na tena ujasiri wa kuota! Amemshukuru mhubiri kwa ujasiri aliouonesha wakati wote wa kipindi cha mafungo! Baba Mtakatifu anakaza kusema, huu ni ujasiri ulioneshwa kwa namna ya pekee na watakatifu kama Francisko Xsaveri, ambaye kwa muda wote wa maisha yake, alitamani kwenda China ili kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu.

Baba Mtakatifu kabla ya kufunga vilago na kurejea tena mjini Vatican akiwa amepanda kati ya mabasi matatu yaliyowabeba yeye pamoja na waandamizi wake, alipata nafasi ya kuwasalimia na kuwashukuru viongozi wakuu wa nyumba ya mafungo hapo Ariccia, nje kidogo ya mji wa Roma. Itakumbukwa kwamba, mafungo haya yalianza Jumapili jioni tarehe 6 Machi 2016 kwa kujikita katika maswali pevu ya Injili na hatimaye, mafungo haya yamehitimishwa kwa tafakari juu ya utume wa Bikira Maria katika kazi ya ukombozi! Je, litakuaje neno hili?

Hapa waamini wanatakiwa kutambua kwamba, imani inajikita katika uhalisia wa maisha yao ya kila siku na kwamba, wanahamasishwa na Mama Kanisa kuhakikisha kwamba, wanaishuhudia, kama kielelezo cha imani tendaji! Padre Ermes Ronchi kwa maelekezo ya Baba Mtakatifu Francisko, amewapatia baraka na rehema kamili, wale wote walioshiriki katika mafungo haya kwani ni sehemu pia ya Maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu, changamoto na mwaliko wa kutubu na kumwongokea Mungu sanjari na kumwilisha imani katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

 

 








All the contents on this site are copyrighted ©.