2016-03-12 15:54:00

Huruma ya Mungu inamwilishwa katika huduma ya upendo!


Huruma ya Mungu na huduma ni mada ambayo Baba Mtakatifu Francisko ameitafakari kwa kina wakati wa Katekesi yake kuhusu maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu, Jumamosi tarehe 12 Machi 2016 ma ra tu baada ya kurejea kutoka Jangwani alikokuwa amejichimbia na waandamizi wake kwa muda wa juma zima! Hii ni tafakari ambayo imejielekeza kwa namna ya pekee katika maadhimisho ya Fumbo la Pasaka, yaani mateso, kifo na ufufuko wa Kristo.

Siku ile iliyotangulia kuteswa kwake, Yesu aliwaosha mitume wake miguu, jambo ambalo halikumfurahisha Mtakatifu Petro kiasi cha kukataa kuoshwa miguu na Yesu. Lakini Yesu akamfafanulia maana yake, akiwataka wafuasi wake kujikita katika huduma ya upendo, kama kielelezo makini cha ushuhuda wa imani inayomwilishwa katika matendo! Yesu ni kielelezo cha hali ya juu kabisa cha Mtumishi wa Mungu, sifa iliyotolewa na Nabii Isaya! Yesu anakuwa kweli ni shuhuda wa huduma ya upendo na kielelezo cha amri mpya ya upendo inayowataka watu kupendana na kwamba, Yesu mwenyewe ameonesha upendo huu hata akawa tayari kuyamimina maisha yake na kwa njia hii watu wamelitambua pendo lake. Ushuhuda wa upendo anakaza kusema Baba Mtakatifu Francisko unapaswa kujikita katika matendo na kweli! Ni huduma ya unyenyekevu inayotekelezwa katika hali ya ukimya kama Yesu mwenyewe anavyowahimiza wafuasi wake kutenda pasi na makuu wala kujikweza!

Huduma ya upendo inajikita anasema Baba Mtakatifu hata katika kugawana mali ya dunia, ili kuwasaidia wenye shida zaidi, kielelezo cha utendaji wa Mungu katika maisha ya mwanadamu. Huu ni ushuhuda wa ubinadamu na utu wema unaopaswa kupewa msukumo wa pekee katika maisha ya watu! Yesu kwa kuwaosha miguu mitume wake, amewataka pia kuungamiana mapungufu yao; kusali na kuombeana, tayari kusamehe na kusahau.

Mtakatifu Augustino, Askofu na mwalimu wa Kanisa anakazia umuhimu wa huduma ya mapendo kwa ndugu na jirani inayowasha mapendo moyoni na kurutubishwa kwa njia ya unyenyekevu. Hii ni chachu ya msamaha na sala inayowasaidia waamini kuoshana dhambi zao kama alivyofanya Yesu kwa kuwaosha miguu mitume wake! Baba Mtakatifu akaza kusema, kuwa na huruma kama Baba maana yake ni kumfuasa na kumshuhudia Kristo katika njia ya huduma ya mapendo! Baba Mtakatifu anawatakia waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema maandamizi mema ya maadhimisho ya Fumbo la Pasaka, yaani mateso, kifo na ufufuko wa Kristo.

Maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu ni kipindi muafaka cha upyaisho wa maisha ya kiroho kwa mtu binafsi na familia yake. Anawataka waamini kuwa kweli ni mashuhuda na vyombo vya huduma ya upendo kwa ndugu na jirani zao, ili kuona mwanga wa maadhimisho ya Fumbo la Pasaka linaloangaza nyoyo za waamini, kielelezo makini cha ushuhuda wa imani tendaji. Waamini wajitahidi kweli kuwa ni mashuhuda wa upendo. Amewataka Majandokasisi kutoka Poland, kuimarishwa kwa namna ya pekee kabisa katika maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu, iliwaweze kuwa waaminifu kwa Kristo kwa kuitikia wito wake kwa moyo wa ukarimu na utayari!

Kwa waamini na mahujaji mbali mbali, Baba Mtakatifu bado anawataka kumwilisha matendo ya huruma kwa ndugu na jirani zao. Vijana wawe makini kusimama kidete ili kulinda na kutetea tunu msingi za maisha ya kiimani; wagonjwa watolee mateso na mahangaiko yao kwa wale wote wanaoteseka na kunyanyasika kutokana na imani yao kwa Kristo na Kanisa lake. Wanandoa wapya washirikiane na Mwenyezi Mungu katika malezi na elimu kwa watoto wao!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.