2016-03-11 06:47:00

SECAM: Haki, amani na upatanisho bado ni changamoto pevu Barani Afrika!


Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika na Magadascar, SECAM katika mkutano wake uliohitimishwa hivi karibuni huko Accra, Ghana linasema, upatanisho, haki na amani ni changamoto endelevu Barani Afrika. Makanisa mahalia pamoja na Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika hayana budi kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha misingi ya haki, amani, maridhiano na majadiliano mintarafu Mafundisho Jamii ya Kanisa.

Haya ni kati ya mambo msingi ambayo SECAM imeyabainisha katika mkutano wa wanne wa Makatibu wakuu wa Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika na Madagascar wakati huu Mama Kanisa anapoadhimisha Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu sanjari na Mwaka wa Upatanisho Barani Afrika; maadhimisho ambayo yanatarajiwa kuhitimishwa hapo tarehe 29 Julai 2016. SECAM inamshukuru na kumpongeza Baba Mtakatifu Francisko kwa kuzindua maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu wakati wa hija yake ya kitume Barani Afrika. Mji wa Bangui, ukawa ni mji mkuu wa huruma ya Mungu duniani!

Makatibu wakuu pamoja na majukumu yao ya kila siku, kwa namna ya pekee, wanahamasishwa na SECAM kuhakikisha kwamba, wanawalinda na kuwaendeleza watoto ili wasikumbukwe na nyanyaso za kijinsia. Umefika wakati kwa Mabaraza ya Maaskofu kuimarisha mchakato wa mawasiliano kwa kutumia kikamilifu maendeleo ya sayansi na teknolojia ya habari, sanjari na matumizi ya mitandao ya kijamii.

Makatibu wakuu wanahimizwa kutunza vyema kumbu kumbu za Kanisa Barani Afrika pamoja na kuendelea kubainisha sera na mikakati itakayowawezesha makatibu wakuu kukutana ili kubadilishana ujuzi, uzoefu na mang’amuzi katika maisha na utume wa Kanisa ili kudumisha umoja na mshikamano wa familia ya Mungu Barani Afrika. Makatibu wakuu watambue kwamba, wao ni wasaidizi wa kwanza wa Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Barani Afrika; viongozi wanaopaswa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa ustawi na maendeleo ya Kanisa Barani Afrika. Makatibu wakuu wa Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika na Madagascar watakutana baada ya miaka mitatu kuanzia sasa huko Zambia.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.