2016-03-11 11:19:00

Burundi wananchi wanataka haki, amani na utulivu!


Baraza la Makanisa Ulimwenguni, WCC, kwa kushirikiana na Baraza la Makanisa Yote Afrika, AACC, hivi karibuni limehitimisha ziara ya mshikamano wa amani nchini Burundi kwa kuzitaka pande zote zinazohusika na mgogoro huu kujikita katika mchakato wa umoja, uponyaji na upatanisho wa kitaifa ili kujenga na kudumisha haki, amani na maridhiano. Katika siku za hivi karibuni, Burundi imeshuhudia machafuko ya kisiasa na kijamii, hali ambayo inahitaji pande zinazohusika kuonesha utashi wa kisiasa utakaojikita katika majadiliano yanayojikita katika ukweli na uwazi, ustawi na maendeleo ya wananchi wote wa Burundi.

Ujumbe wa viongozi wa Makanisa unasema, wahusika waweke silaha zao chini; sheria ianze kuchukua mkondo wake, ili wale wanaovunja sheria waweze kushughulikiwa kikamilifu katika ukweli na haki sanjari na kuheshimu Mkataba wa amani, uliotiwa sahihi kunako mwaka 2000 mjini Arusha na huo ukawa ni mwanzo wa ukurasa mpya nchini Burundi iliyokuwa imetikiswa na kuguswa na vita ya wenyewe kwa wenyewe kwa kipindi cha miaka kumi na miwili. Viongozi wa Serikali na upinzani wanahamasishwa kujifunga kibwebwe ili mchakato wa amani ushike kasi, hatimaye, kujenga umoja na mshikamano wa kitaifa.

Dr. Olav Fyske Tvait anafupisha ziara yao ya mshikamano nchini Burundi kwa kusema, viongozi wa Makanisa wameisikiliza kwa makini Familia ya Mungu nchini Burundi; wamezungumza na wadau mbali mbali katika mgogoro huu na kwamba, wote wameonesha kiu ya kutaka kujenga na kudumisha haki, amani na maridhiano sanjari na kuendeleza majadiliano ya kitaifa. Huu ni wakati wa kuhakikisha kwamba, kiu na matamanio haya ya familia ya Mungu nchini Burundi yanafanyiwa kazi.

Kuna uvunjwaji mkubwa wa haki msingi za binadamu unaoendelea kutendeka nchini Burundi, mwaliko wa kuanza mchakato wa majadiliano ili kujenga na kudumisha haki, amani na maridhiano kati ya wananchi wa Burundi. Ukabila hauna nafasi tena, ukiendekezwa, Burundi itatumbukia tena kwenye maafa makubwa. Amani na utulivu virejee, ili kutoa nafasi kwa wapinzani kurejea nchini mwao ili kushiriki katika ujenzi wan chi kwa kuyatafutia ufumbuzi matatizo na changamoto za Burundi kwa nyakati hizi kwa njia ya amani, kwani Burundi itajengwa na wananchi wenyewe!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PPS.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

 

 








All the contents on this site are copyrighted ©.