Baraza linalo waunganisha Maaskofu Katoliki katika Mkoa wa Afrika Kati( ACERAC) limeomba amani, maelewano na umoja wakati wote wa michakato ya uchaguzi wa Rais, kipindi kinachopita sasa katika nchi nyingi za mkoa huo. Baraza hilo huunganisha Maaskofu Katoliki kutoka Cameroon, Congo Brazzaville, Gabon, Jamhuri ya Afrika ya Kati, Chad, Guinea ya Ikweta. Habari inabaini , ombi la ACERAC , lilitolewa mwishoni mwa Mkutano wa Baraza hilo, uliofanyika mjini Brazzaville, mji mkuu wa Jamhuri ya Kongo.
Taarifa tokea baraza hilo inaendelea kusema, Maaskofu,wamepokea kwa mikono miwili na shukurani nyingi kwa mwenendo wa amani uliyoonekana katika uchaguzi wa hivi karibuni katika Jamhuri ya Afrika ya Kati na wamemshukuru Papa Francisko , kwa mchango wake alioutoa kwenye mshikamano wa kitaifa , wakati wa ziara yake ya mwezi Novemba mwaka jana. ACERAT, inahimiza juhudi hizi zilizofanyika Car pia iwe ni somo kwa mataifa mengine ya Afrika Kati. Na wameonyesha kujali hali za wasiwasi na vitisho vinavyojionyesha katika baadhi ya mataifa kwa kadri siku za uchaguzi zinavyokaribia. Wameendelea kuomba ujasiri wa kushinda changamoto zinazowakabili kwa njia y amani na maelewano badala ya kutumia vurugu. Wameonyesha pia kutambua kwamba, kuna matatizo yanayokera raia , mfano tatizo la ukosefu wa ardhi na mgogoro wa kiuchumi na kifedha, na hali zingine zenye kusababisha maisha magumu kwa watu wengi wakati wachache kati yao wakineemeka na utajiri wa kitaifa.
Pamoja na matatizo hayo , bado ni muhimu kuandaa uchaguzi wenye kuheshimu demokrasia na sheria , kama uhakika wa kuwa na usawa na fursa ya wote kushiriki kama haki yao ya kikatiba. Kwa hili, wamekumbusha umuhimu na haja ya kuangalia maslahi ya umma na kukuza manufaa ya wote,. Hivyo wameomba amani, umoja na maelewano kwa watu wote, wake kwa waume katika Mkoa wa Afrika ya Kati na majirani zake.
All the contents on this site are copyrighted ©. |