2016-03-09 08:24:00

Mkakati wa COMECE: Ukarimu na amani!


Kutokana na changamoto mbali mbali zinazoendelea kujionesha kwenye mipaka ya Nchi mbali mbali Barani Ulaya, kuna haja ya kujenga na kudumisha utamaduni wa ukarimu, haki na amani, ili kuweza kuwapokea na kuwahudumia wakimbizi na wahamiaji wanaoendelea kuteseka kutokana na baridi, njaa na utupu. Hawa ni watu wanaokimbia vita, njaa na umaskini; wanatafuta amani na hifadhi ya maisha. Umoja wa Ulaya unapaswa kuwa na sera na mikakati makini ya kuwapokea, kuwahudumia na kuwaingiza wakimbizi na wahamiaji katika maisha ya wananchi wake, ili waweze kushiriki katika mchakato wa maendeleo na ustawi wa wengi

Juhudi hizi hazina budi kwenda sanjari na mchakato utakaoiwezesha Jumuiya ya Ulaya kuwa na sera na mikakati ya muda mrefu kwa ajili ya kusaidia kukuza na kudumisha haki, amani na maendeleo katika nchi ambazo kuna idadi kubwa ya wakimbizi na wahamiaji wanaoendelea kubisha hodi Barani Ulaya na huko wanakumbana na pazia la chuma! Haya ndiyo yaliyopewa uzito wa pekee na viongozi wa Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Jumuiya ya Ulaya, COMECE katika mkutano wake uliokuwa unafanyika hivi karibuni mjini Brussels, Ubelgiji. Mkutano huu umeongozwa na dhamiri “Utume wa Bara la Ulaya kuendeleza Amani Duniani”. Tema hii inagusa hali halisi ya changamoto zinazoendelea kujitokeza Barani Ulaya kutokana na wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji kutoka Mashariki ya kati wanaotaka kupewa hifadhi na usalama wa maisha Barani Ulaya.

Kutokana na changamoto hizi, Kanisa linahamasishwa kushiriki kikamilifu katika mchakato wa kujenga na kudumisha amani ndani na nje ya Bara la Ulaya. Mkutano huu pamoja na mambo mengine, umejadili kwa kina na mapana kuhusu: amani, uhusiano kati ya Nchi za Jumuiya ya Ulaya ambao kwa siku za hivi karibuni umelegalega kutokana na changamoto ya wahamiaji inayozifanya nchi hizi kufunga mipaka yake. Wakimbizi, haki msingi za binadamu na kanuni maadili katika masuala ya kibaiolojia.

Jumuiya ya Ulaya haina budi kushiriki kikamilifu katika mchakato wa ujenzi wa misingi ya haki, amani na maridhiano kati ya watu ndani na nje ya Ulaya, dhana iliyopewa mkazo na waasisi wa Umoja wa Ulaya. Katika kipindi hiki kigumu, Umoja wa Ulaya hauna budi kuonesha ushirikiano na mshikamano na nchi nyingine duniani ili kuweza kukabiliana na changamoto zinazomwandama mwanadamu katika ulimwengu mamboleo. Jumuiya ya Ulaya itekeleze dhamana na wajibu wake katika medani mbali mbali za kimataifa.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.