2016-03-09 14:13:00

Jina la Mungu ni huruma!


Kitabu kiitwacho “Jina la Mungu ni Huruma” (The name of God is Mercy) ni matunda ya mazungumzano kati ya Baba Mtakatifu Francisko na Andrea Tornielli. Ndani mwake Baba Mtakatifu anaelezea juu ya ukuu wa huruma ya Mungu dhidi ya dhambi ya mwanadamu. Katika moja ya mazungumzo hayo Baba Mtakatifu Francisko anaonesha ukuu wa huruma ya Mungu dhidi ya hukumu yake. “Kunapokuwa na huruma, hukumu inakuwa ni ya haki zaidi na inatimiza uhalisia wake ... tunapaswa kuwasaidia wale walioanguka ili warudi. Mara nyingi tunapendelea kumfungia mtu magerezani kwa maisha yote badala ya kujaribu kumkarabati na kumsaidia kuitafuta nafasi yake ndani ya jamii”. Kwa utangulizi hii mfupi nakualika katika Dominika hii ya tano ya Kwaresima kutafakari juu ya hukumu ya Mungu inayojengwa katika Upendo wake.

“Kwa nini Mungu hachoki kutusamehe” anauliza Tornielli. Baba Mtakatifu Francisko anamjibu: “ Kwa sababu ni Mungu, kwa sababu yeye ni huruma na kwa sababu huruma ni sifa ya kwanza ya Mungu. Huruma ni jina la Mungu”. Sura hii ya Mungu inafunuliwa na Kristo katika tukio tunalolisikia katika Injili ya leo. “Wala mimi sikuhukumu. Enenda zako; wala usitende dhambi tena”. Ukiangayaangalia kwa haraka maneno haya ya Yesu yanaonesha kwamba hakutaka kumhukumu. Ila sentesi ya mwisho “usitende dhambi tena” inaonesha namna ambavyo hukumu ya Mungu inakuja kwetu katika hali ya upendo. Inakuja kwetu kwanza kwa kutambua kwamba umekosa, kwamba umetenda dhambi lakini inakwenda hatua moja zaidi kwa kuelekeza kutorudi katika hiyo hali ya dhambi. Waandishi na Mafarisayo walibaki katika hali ya kuhukumu na kutotoa nafasi ya huyu mama kutubu na kuongoka.

Sheria ya Musa kama ilivyoelekezwa na kitabu cha Torati inasema kwamba: “akifumaniwa mtu mume amelala na mwanamke aliyeolewa na mume na wafe wote wawili, mtu mume aliyelala na yule mwanamke, na yule mwanamke naye” (Kumb 22:22). Kristo hakuonesha kuipinga sheria hii wala kukubaliana nayo. Anawataka wao kutafakari juu ya matendo yao maovu na si tendo uzinzi tu, anawataka wao kuona ukubwa wa uhasi wao kwa Mungu. Uadilifu wao ndiyo uwahalalishe wao kumpiga kwa mawe. Katika Agano la kale taifa la wana wa Israeli walihukumiwa kama wazinzi pale walipohamishia mapenzi yao kw miungu mingine na siyo kwa Mungu, yaani, pale walipokuwa wadhambi (Rej Ezek 16: 38, 40). Mwanadamu anawakilishwa hapa na taifa la Israeli. Mungu anatutendea mema mengi,anatumiminia fadhila zake kila uchwapo lakini majibu yetu ni uhasi na kupoteza uhamifu kwake.

Kristo anapowataka Mafarisayo na waandishi kufikia katika kuiona hali hiyo kwamba shida si tendo la uzinzi bali matokeo ya tendo hilo, yaani dhambi inayomtenganisha mwanadamu na Mungu anatukumbusha na sisi leo tunapohukumu wengine: “asiye na dhambi miongoni mwenu awe wa kwanza wa kumtupia jiwe”. Wao pamoja na kushadadia kuuwawa kwa mama huyu sababu ya uzinzi wanashindwa kuona nao uhasi wao kwa Mungu sababu kwa dhambi zao. Kwa maneno mengine wao wanakuwa wepesi kuona kibanzi katika jicho la mwenzao na si boriti katika jicho lao. Katika kitabu “Jina la Mungu ni Huruma, Baba Mtakatifu anasema kwamba “mmoja anaweza kuwa mdhambi mkubwa sana lakini asiangukie katika udhalimu ... huyu anajifunua katika msamaha wa Mungu na moyo wake huisi udhaifu wake wenyewe na huko kujifunua kidogo huruhusu huruma ya Mungu ipenye ... mtu aliye mdhalimu mara nyingi hajitambui hali yake kama mtu anayeshindwa kuitambua harufu mbaya inayotoka mwilini mwake”.  Huruma ya Mungu ni kubwa kuliko hukumu yake. Kristo ambaye alibaki peke yake pamoja na huyu mshitakiwa alikuwa na uhalali wa kumhukumu. Kati ya wote waliokuwa pale ni Yeye peke yake ambaye alikuwa katika mstari ulio sawa. Hapa anaufunua ukuu wa huruma ya Mungu iliyojengeka katika upendo wake: “Wala mimi sikuhukumu. Enenda zako; wala usitende dhambi tena”.

Mwenyezi Mungu daima anajenga na anatafuta kuokoa. Mtakatifu Masimo muungama anavyoelezea huruma ya Mungu kwa anayetubu anasema: “Mfano wa sarafu iliyopotea (rej. Lk 15:8 – 10) Kristo anarejea katika lugha ya picha katika ukweli kwamba amekuja kumrejesha tena mwanadamu ile hadhi ya kifalme ambayo ilipotezwa harufu mbaya ya uovu”. Sisi wanadamu kinyume chake tunatafuta kujenga kwetu na kubomoa kwa wengine, tuko wepesi kuona uovu wa wenzetu na si namna ya kuwatoka katika magumu yanayowasibu. Katika somo la kwanza Nabii Isaya anaifafanua huruma hii kuu ya Mungu. Mungu anawarudishia wana wa Israeli hadhi yao waliyoipoteza na anaahidi kuendelea kuwategemeza: “Tazama nitatenda neno jipya ... nitafanya njia hata jangwani na mito ya maji nyikani”. Huyu ndiye Mungu wetu ambaye jina lake ni huruma. Hakika anatupatia nguvu ya kuimba pamoja na mzaburi kwamba “Bwana alitutendea mambo makuu, tulikuwa tukifurahi”.

Mtume Paulo katika somo la pili anatupatia wito wa kubaki katika upya huo ambao tunaupokea kutoka kwa Mungu. Ni kana kwamba maneno yale ya Kristo “usitende dhambi tena” yanajirudia kwa namna nyingine na huu ndiyo wito wetu wa maisha ya kikristo. Paulo anaendelea kufafanua kwamba ukristo wetu unapaswa kukua au kuimarika ili kufikia ukamilifu katika Kristo. “Si kwamba nilikwisha kufika, au nimekwisha kuwa mkamilifu; la! Bali nakaza mwendo ili nipate kulishika lile ambalo kwa ajili yake nimeshikwa na Kristo Yesu”. Ni wito wa kuendelea kuyaimarisha maisha yetu ya utumishi ili kufikia ukamilifu na hata kukariri kama Mtume na kusema “nimepigana vita vilivyo vizuri, mwendo nimeumaliza na imani nimeilinda”.

Nakualika katika Dominika ya leo kujinyenyekeza mbele ya Mungu katika hali ya toba na kuomba msamaha kwake mithili ya yule mtoza ushuru hekaluni: “Ee Mungu! Unihurumie mimi ni mwenye dhambi!”. Tuepuke tabia za kujikuza na kujikinai katika haki huku tukiwatupa wenzetu katika nafasi ya wadhambi na wazinzi ambao hawawezi kupata nafasi kwa Mungu. Baba Mtakatifu Francisko anaonya kwamba ni afadhali ya mtu mdhambi ambaye anatubu kuliko yule dhalimu ambaye hujiona hana dhambi. Huruma ya Mungu ni kubwa kuliko wingi wa dhambi zako. Mungu anahukumu katika hali ya upendo. Yeye anatafuta kukujenga upya na kukuondoa katika utumwa wa dhambi. Leo hii unapomwendea kwa moyo wa toba katika huruma yake hiyo kuu anakuambia hata wewe: “Enenda zako, wala usitende dhambi tena”. Anakutaka uende na kuimarika katika ufuasi wako.

Tafakari hii imeletwakwako na Padre Joseph Peter Mosha.








All the contents on this site are copyrighted ©.