2016-03-09 09:23:00

Angola Jubilei ya miaka 525 ya Imani; Miaka 150 ya Uinjilishaji awamu ya Pili


Baraza la Maaskofu Katoliki Angola, Sao Tomè na Principe tangu tarehe 2 hadi 9 Machi 2016 linafanya mkutano wake wa mwaka huko Ndalatando, mkoani Kwanza Notre. Kati ya mambo makuu yanayojadiliwa kwa sasa ni majiundo endelevu ya mihimili ya Uinjilishaji nchini Angola; mbinu mkakati wa kuimarisha matangazo ya Radio Ecclesia ili iweze kutoa huduma kwa nchi nzima pamoja na maandalizi ya mkutano mkuu wa Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Kusini mwa Afrika, IMBISA utakaofanyika mwezi Novemba, huko Lesotho. Kanisa Katoliki nchini Angola linajiandaa pia kwa ajili ya maadhimisho ya Kongamano la Kikanisa litakaloadhimishwa Jimbo kuu la Huambo, Angola.

Katika hotuba yake ya ufunguzi, Askofu mkuu Filomeno do Nascimento Vieira Dias, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Angola, Sao Tomè na Principe, CEAST amekazia kwa namna ya pekee maadhimisho ya Kongamano la Kikanisa Kitaifa nchini Angola kama sehemu ya maadhimisho ya Jubilei ya miaka 525 tangu imani ya Kikristo ilipoingia nchini Angola na Jubilei ya miaka 150 ya Uinjilishaji awamu ya pili nchini Angola. Hiki ni kipindi cha kumtafuta na kumwambata Yesu Kristo, ukweli, njia na uzima sanjari na kujiimarisha katika kutembea kwenye njia ya Injili.

Kwa upande wake, Askofu mkuu Josè Manuel Imbamba amekumbushia kwamba, mwaka 2016 ni kilele cha Uinjilishaji wa kina uliovaliwa njuga na Maaskofu katika kipindi cha miaka mitatu kama sehemu ya maadhimisho ya Jubilei ya 150 ya Uinjilishaji wa awamu ya pili nchini Angola. Kipindi hiki ni wakati muafaka wa kutoa dira na mwelekeo wa shughuli za kichungaji katika kipindi cha miaka miatatu kuanzia mwaka 2017 hadi mwaka 2019.

Familia ya Mungu nchini Angola inatumia fursa hii kuonesha upendo na mshikamano na viongozi wao wa Kanisa kwa kusali na kuwasindikiza katika maisha na utume wao, ili waweze kusoma alama za nyakati na kutambua changamoto zinazolikabilia Kanisa kwa nyakati hizi, tayari kuzipatia majibu muafaka kwa njia ya mwanga wa Injili ya Kristo. Baraza la Maaskofu Katoliki Angola, Sao Tomè na Principe linakutana mara mbili kila mwaka; mara ya kwanza linakutana mjini Luanda na awamu ya pili linakutana mbali kidogo, ili kuweza kufahamu hali halisi ya Kanisa pembezoni mwa jamii!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.