2016-03-08 08:03:00

Uandishi wa habari nyakati za Papa Francisko!


Changamoto za tasnia ya habari nyakati za uongozi wa Baba Mtakatifu Francisko ni mada ambayo imechambuliwa hivi karibuni katika kongamano la Shirikisho la Waandishi wa Habari Wakatoliki nchini Italia. Kongamano hili limeadhimishwa hivi karibuni huko Matera, nchini Italia. Katika nyakati hizi za maendeleo ya sayansi na teknolojia ya habari, wajibu wa mwandishi wa habari si kuwa wa kwanza kutoa habari, bali kuhakikisha kwamba, anatoa habari sahihi kwa kuhakiki vyanzo vyake vya habari na kuiweka habari yenyewe mahali pake na kuipatia tafsiri sahihi, ili habari hii iweze kuwa ni kumbu kumbu katika historia ya jamii iliyostaarabika.

Kanuni maadili, sheria na taratibu za uandishi wa habari ni mambo ya kuzingatiwa na wadau mbali mbali katika tasnia ya habari kama alivyowahi kukazia Mwenyeheri Paulo VI katika hotuba zake za kwanza kwanza kwa waandishi wa habari! Uandishi wa habari ni tasnia inayokita huduma yake katika ujasiri, ukweli, demokrasia, maendeleo, ustawi na mafao ya hadhira inayokusudiwa. Ni huduma inayotoa sauti kwa watu wasiokuwa na sauti kama anavyosisitizia Baba Mtakatifu Francisko.

Habari inayotolewa inapaswa kusheheni ukweli kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa binadamu na mahitaji yake msingi. Waandishi wa habari wanapaswa kusimama kidete kulinda na kutetea utu na heshima ya binadamu dhidi ya ukosefu wa haki msingi za binadamu na mambo yote yanayodhalilisha utu wake! Hii ni changamoto iliyotolewa na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican wakati wa Kongamano la Shirikisho la Waandishi wa Habari Wakatoliki nchini Italia. Anakaza kusema, umuhimu na uzito wa habari unategemea kwa kiasi kikubwa: ukweli wote na uaminifu katika kudumisha demokrasia, ustawi na maendeleo ya binadamu.

Uandishi bora unaweza kusaidia kukuza na kudumisha demokrasia ya kweli ndani ya jamii kwa kuanzisha majukwaa ya watu kukutana na kusikilizana; kwa kuheshimiana na kuthaminiana hata katika tofauti zinazoweza kujitokeza; kwa kujenga na kudumisha umoja na mshikamano kwa mambo yanayowaunganisha wote; kwa kutoa habari zisizoegemea upande mmoja, kwa kuwashirikisha wadau mbali mbali, ili ukweli uweze kuonekana!

Kuna mahusiano makubwa kati ya demokrasia na mawasiliano yanayojikita katika huduma kwa jamii licha ya kuangalia mwelekeo wa kiufundi na kiteknolojia. Ubora na ukweli wa habari ni muhimu sana anasema Baba Mtakatifu Francisko katika Ujumbe wake wa Siku ya 50 ya Mawasiliano Duniani kwa Mwaka 2016. Ulimwengu wa digitali ni mahali pa watu kukutana, hapa watu wanaweza kuonja upendo, au kupata majeraha ya kudumu katika maisha yao; watu wanaweza kujadiliana kwa ajili ya mafao ya wengi lakini pia inaweza kuwa ni mahali ambapo wengi wanakengeuka na kupotoka kimaadili.

Uhuru wa watu kujieleza unapaswa kuheshimiwa, lakini pia usindikizwe na kanuni maadili na utu wema. Waandishi wa habari wanaweza kusaidia kuelimisha mchakato wa upatanisho kati ya watu, ili amani ya kudumu iweze kupatikana, ili iweze kujikita katika akili na mioyo ya watu! Kuna mabadiliko na maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia ya habari, dhana ambayo imevaliwa njuga na viongozi mbali mbali wa Kanisa kuanzia mwaka 1931 Papa Pio wa kumi na moja alipotangaza kwa mara ya kwanza kupitia Radio.

Kunako mwaka 1953 kwa mara ya kwanza Papa Pio XII akaoneka kwenye Luninga. Tarehe 3 Desemba 2012 Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto XVI akatuma ujumbe wake wa kwanza kwa njia ya twitter. Katika maadhimisho ya Siku kuu ya Ekaristi Takatifu kwa mwaka 2014, Baba Mtakatifu Francisko aliungana na Majimbo 500 duniani, ili kuadhimisha kutafakari Fumbo la Ekaristi Takatifu. Mawasiliano ni nyenzo muhimu ya ujenzi wa umoja, udugu na urafiki, kumbe hapa changamoto ni kuwa waaminifu kwani hapa watu wanashirikishana pia utu na heshima yao kama binadamu!

Mwandishi wa habari Mkatoliki anapaswa pia kushuhudia imani yake katika shughuli zake za kila siku. Huu ni wajibu ambao umeshuhudiwa na viongozi mbali mbali wa Shirikisho la Waandishi wa Habari Wakatoliki nchini Italia tangu mwaka 1959. Wamekuwa ni chachu ya majadiliano kati ya Kanisa na Ulimwengu mamboleo changamoto iliyotolewa na Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican. Hapa kuna haja ya kuwekeza katika majiundo ya waandishi wa habari, ili kuwapatia nafasi ya kutekeleza dhamana na wajibu wao kwa ufanisi mkubwa anasema Kardinali Parolin sanjari na kukazia mwelekeo mpya wa mawasiliano ndani ya Kanisa.

Itakumbukwa kwamba, kunako tarehe 12 Juni 2010, Kanisa lilimtangaza Manuel Lozano Garrido, mwamini mlei kuwa Mwenyeheri, aliyetekeleza wajibu wake wakati wa vita ya wenyewe kwa wenyewe nchini Hispania. Kwa miaka 28 alikuwa kilema, lakini bado akaendelea kuchapa kazi ya uandishi wa habari, leo hii ni mfano bora wa kuigwa. Aliwataka waandishi wa habari kuwa waaminifu, kwa kutekeleza dhamana yao katika ukweli na uwazi, imani na matumaini ya maisha ya uzima wa milele!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.