2016-03-08 12:18:00

Sipati picha na huruma ya Baba!


Mfano huu wa Yesu kwa karne nyingi tulizoea kuupatia kichwa cha habari - ‘Mfano wa Mwana Mpotevu”. Siku hizi, hasa baada ya Mt. Yohane Paulo II alipoandika waraka wake wa kichungaji yake ‘Dives in Misericoridia’ (Tajiri wa Huruma) na Mapapa waliofuata, hasa Baba Mtakatifu Francisko, Mfano huu tunauita Mfano wa Baba wa Huruma. Tuusome tena taratibu Mfano huu na kuutafakari kwa kina utajiri wa ujumbe unaoletwa kwetu na Injili hii Takatifu:

I - Injili ya Luka 15:11-32:

“Akasema, Mtu mmoja alikuwa na wana wawili; yule mdogo akamwambia babaye, Baba, nipe sehemu ya mali inayoniangukia. Akawagawia vitu vyake. Hata baada ya siku si nyingi, yule mdogo akakusanya vyote, akasafiri kwenda nchi ya mbali; akatapanya mali zake huko kwa maisha ya uasherati. Alipokuwa amekwisha tumia vyote, njaa kuu iliingia nchi ile, yeye naye akaanza kuhitaji. Akaenda akashikamana na mwenyeji mmoja wa nchi ile; naye alimpeleka shambani kwake kulisha nguruwe.Akawa akitamani kujishibisha kwa maganda waliyokula nguruwe, wala hapana mtu aliyempa kitu. Alipozingatia moyoni mwake, alisema, Ni watumishi wangapi wa baba yangu wanaokula chakula na kusaza, na mimi hapa ninakufa kwa njaa.

Nitaondoka, nitakwenda kwa baba yangu na kumwambia, Baba, nimekosa juu ya mbingu na mbele yako; sistahili kuitwa mwana wako tena; nifanye kama mmoja wa watumishi wako. Akaondoka, akaenda kwa babaye. Alipokuwa angali mbali, baba yake alimwona, akamwonea huruma, akaenda mbio akamwangukia shingoni, akambusu sana. Yule mwana akamwambia, Baba, nimekosa juu ya mbingu na mbele yako; sistahili kuitwa mwana wako tena. Lakini baba aliwaambia watumwa wake, Lileteni upesi vazi lililo bora, mkamvike; mtieni na pete kidoleni, na viatu miguuni; mleteni ndama yule aliyenona mkamchinje; nasi tule na kufurahi; kwa kuwa huyu mwanangu alikuwa amekufa, naye amefufuka; alikuwa amepotea, naye ameonekana. Wakaanza kushangilia.

Basi, yule mwanawe mkubwa alikuwako shamba na alipokuwa akija na kuikaribia nyumba, alisikia sauti ya nyimbo na machezo. Akaita mtumishi mmoja, akamwuliza, Mambo haya, maana yake nini? Akamwambia, Ndugu yako amekuja, na baba yako amemchinja ndama aliyenona, kwa sababu amempata tena, yu mzima. Akakasirika, akakataa kuingia ndani. Basi babaye alitoka nje, akamsihi. Akamjibu baba yake, akasema, Tazama, mimi nimekutumikia miaka mingapi hii, wala sijakosa amri yako wakati wo wote, lakini hujanipa mimi mwanambuzi, nifanye furaha na rafiki zangu; lakini, alipokuja huyu mwana wako aliyekula vitu vyako pamoja na makahaba, umemchinjia yeye ndama aliyenona. Akamwambia, Mwanangu, wewe u pamoja nami sikuzote, na vyote nilivyo navyo ni vyako. Tena, kufanya furaha na shangwe ilipasa, kwa kuwa huyu ndugu yako alikuwa amekufa, naye amefufuka; alikuwa amepotea, naye ameonekana..”

1. Kuvuka mipaka ya fidia ya haki

Mbele yetu tunalo Simulizi la Yesu ambalo kama fundo kubwa. Namna za kulipangua na kulifungua ni nyingi. Itabidi tuchague njia ambayo inajitokeza kama njia kuu ya kufumbua maana halisi ya Mfano huu wa Baba wa Huruma. Njia hii ni - kupokea au kutoa fidia ya haki. Tangu mwanzo wa Simulizi hili, Yesu anasisitiza kwamba kulipwa stahili za haki ni sehemu muhimu ya haki za kimsingi za kibinadamu. Baba katika Simulizi anao wana wawili. Mdogo anamuuliza Babaye stahili zake za urithi ni kiasi gani maana anataka azitwae bila kusubiri kifo cha Babaye na sheria za mirathi, za urithi kuchukua mkondo wake. Hatuambiwi katika Simulizi hili ni nini kilichomfanya kijana huyo kuchukua uamuzi huo? Yesu hafafanui, ananyamazia makusudi yao ili wasikilizaji wake wasitawanye mawazo bali wayalenge yaliyo ya msingi na muhimu katika Simulizi lake.

Baba anakubali dai la mwanaye na anawagawia wote wawili urithi wake. Sasa,  sheria ya kugawa mali ya Mzee ilitawaliwa na Sheria ya Kiyahudi ya wakati ule wa Yesu. Kwa mujibu wa Sheria hiyo (tunasoma katika Kitabu cha Kumbukumbu la Torati 21:17) kifungua mimba - mwanaye wa kwanza alitakiwa apokee theluthi mbili za urithi kutoka kwa Babaye. Na mdogo wake - theluthi moja iliyobakia. Kinachotukwaza hapa ni ukweli kwamba urithi ulikuwa unagawanywa kati ya watoto wa mhusika baada ya kifo chake, na si wakati wa uhai wake!

Teso la kwanza la moyo wa Baba katika Simulizi hili ni kitendo cha kijana wake cha kutosubiri kifo cha Babaye bali kudai sehemu ya mali iliyomwangukia kisheria wakati wa uhai wa Baba. Kwa kifupi, kwa kijana huyo mali ilikuwa na thamani kubwa zaidi kuliko hata uhai wa Babaye! Kwa kitendo chake hicho wazi cha tamaa ya mali na kutumikia tamaa zake za kimwili na uhuru feki wa maisha - kijana alionyesha wazi kwamba kwake Baba yake si kitu tena, ni sawa na kumuua na kumzika tayari katika fikra zake na moyoni mwake. Uhusiano wa kijana na Baba yake ulikatishwa hapo na kufa moja kwa moja. Kijana alifisha uhusiano wake na Baba. Kwake Baba alikufa amekwishakufa. Teso kali kwa moyo uliojaa upendo na huruma wa Baba! Kwa upande wa kijana mkubwa mambo si mazuri pia. Baba aliwagawia wote wawili urithi na mali zake zote. Mdogo kaondoka, mkubwa kabaki akiwa msimamizi wa mali zote za Baba zilizobaki ambazo sasa zilikuwa zake. Baba hana mali tena.

Kwa kijana mkubwa, Baba ni kama amekufa tayari. Si waligawana mali zake – hatua  ambayo inafanyika baada ya kifo cha mwenye mali! Kijana mkubwa alisimamia vizuri bila shaka mali zote zilizomwangukia lakini tutakavyoona katika matashi yake, hakujihesabu tena kama mtoto wa Baba, bali kama mfanyakazi. Kijana mdogo kasafiri na tunavyosoma katika Simulizi - alitapanya mali zake zote kwa maisha ya ufuska, uasherati na matumizi ya hovyo hovyo. Sheria ya stahili za haki inasema wazi kwamba endapo kijana huyo angeamua kurudi nyumbani kwa Babaye, asingestahili kupewa tena kitu chochote. Huenda angeweza kubahatika kusamehewa na Baba maovu yake lakini kwa vile sehemu ya mali iliyokuwa haki yake kisheria alikuwa amekwishapewa na kuitumia, basi, hapa hana misingi yoyote ya kudai kitu chochote tena.

Katika Simulizi la Yesu, sheria ya mirathi inavurugwa kabisa tangu mwanzo mpaka mwisho. Baba hafuati sheria hiyo kwa sababu ni mwingi wa Huruma na havumilii kabisa kali ya mwanaye mdogo! Baba hakai nyumbani akiwasubiri wanawe wote wawili. Mdogo anaporejea nyumbani, anampokea nje maana alikimbia kumpokea, na wala hakumtukana, kumkasirikia, kuuliza mali iko wapi na alikuwa anafanya nini huko kote bila hata mawasiliano na watu wa nyumbani. Badala yake anaamua kumpokea kifalme na kumfanyia karamu kubwa.

Tukumbuke kwamba, Baba hapo alipo hana mali yake mwenyewe (maana aliheshimu uamuzi wake mwenyewe wa kuwagawia mali zake zote na japo angeweza kufuta uamuzi huo na mgawanyo huo kwa vile alikuwa bado hai na ilikuwa ni haki yake ya kubadilsha wosia wake yeye mwenyewe - hakufanya hivyo, akabaki na msimamo ule ule), labda kama aliendelea kuanzisha biashara au ufugaji au kilimo, lakini habari hizi hatuna katika Simulizi, hivyo tunaweka kusema kwamba Baba aliishi kwa kutunzwa na kijana wake mkubwa. Kumbe, Baba kwa ajili ya Ukuu wa Huruma yake, aliamua kujitawala na kutumia mali ya kijana wake mkubwa! Na wala hasubiri kijana huyo arejee nyumbani kutoka shambani ili ashauriane naye wafanye nini na yule mdogo na wamchukulie hatua gani ama waamue nini? Hapana!

Baba anaamua kuchukua hatua za huruma na upendo mara moja akijua moyoni mwake kwamba mwanaye aliyebaki nyumbani atakuwa na huruma na furaha iyo hiyo kama Baba. Kumbe! Kijana alionyesha tabia na msimamo tofauti kabisa na Baba! Kijana mkubwa anaporudi nyumbani, kama ilivyokuwa katika kumpokea mdogo nje ya mji, Baba anakutana naye vile vile nje ya mji na kumbembeleza kijana aliyeshikwa hasira - kwa ajili ya Baba na kwa ajili ya mdogo wake! Na anakataa kujiunga na sherehe ya furaha na shangwe kwa ajili ya mdogo kurejea salama nyumbani.

Kumbe, Baba ni tofauti kabisa na wanawe wote wawili. Mdogo anarudi nyumbani si kwamba anampenda Baba yake na ana majuto ya kweli na ndiyo sababu inayomfanya aache maisha yale ya hovyo. Wala! Mdogo anarudi nyumbani kwa sababu hana kitu, ana njaa, na anatafuta hata kibarua ili mateso yake yaishe. Harudi kwa Baba kwa sababu aliumiza moyo wake, kwa sababu anataka kuhuisha uhusiano wa upendo wa mwana na Baba. Wala! He has no other way out of his problems. Hana njia nyingine. He does care about the Father. It is not his priority. He just thinks about himself and his problems. And the Father is the best solution under the circumstances. Lakini pamoja na hayo hana nia ya kuhuisha uuhusiano wake na Baba.

Kumfufua Baba katika ulimwengu wa maisha yake. Anataka tu kazi, chakula na malazi. Mchoyo. Kijana mkubwa vile vile - mtiririko wa fikra, msimamo na mawazo yake ni kudai kila mtu apate na atendewe kadiri anavyostahili kwa matendo yake. Mfumo huu wamalipo, stahili na fidia ya haki - unamzuia amwone Baba kama Baba yake mwenye Huruma na mdogo wake kama mdogo wake kweli aliyepigika na anahitaji huruma (maana) anapomlaumu Baba hamwiti mdogo wake - mdogo wangu - bali ‘huyu mwana wako’. Msamiati huu unafana kabisa na kauli ya Adamu katika Bustani ya Edeni alipomlaumu Mungu kwa kumpa Hawa aliyemshawishi kula tunda lililokatazwa! Kauli hii ni athari ya dhambi kubwa aliyotenda Adamu na iliyomfanya asiweze kumwona Mungu tena kama Baba aliye na uhusiano wa karibu na wanawe, badala yake dhambi ilimfanya amwogope Mungu na kujificha mbele ya Uso wake wa Huruma).

Kijana anayefanana kabisa na Adamu aliyetenda dhambi ya asili anamkasirikia Baba kwamba alimpokea mdogo wake, mwana mpotevu, mtu asiyefaa na asiyestahili huruma yoyote bali atendewe kadiri ya sheria ya haki. Anamkasirikia Baba kwamba amejitawala na kuchukua katika mali zake ili amfanyie sherehe bwana mdogo hata kama Baba bado ni hai na ni haki yake kisheria kupangua wosia na uamuzi wa mirathi. Kijana mkubwa haoni hilo. Yeye anamwona Baba kama amekwishakufa na hana maamuzi yoyote na uhuru wowote wa kuamua na kutenda. Anamkasirikia Baba kwa huruma yake aliyoonesha. Anamlaumu Baba kwamba hakumfanyia sherehe yeye na rafiki zake wakati amesahau  kwamba mali zote nyumbani ni zake na anaweza kufanya anavyotaka.

Kumbe, naye ni mchoyo na lugumya! Sawa na wazee wengi wanaotunzunguka mkoa huu wa Mara na hapa Kiabakari. Ng’ombe na mbuzi anazo lakini atoe hata mmoja kwa ajili ya kumsomesha mtoto wake vizuri - hakuna! Tunaweza kujiuliza katika kusoma na kutafakari Simulizi hili kwa nini hatumwoni Mama hapa? Mke wa Baba wa Huruma na Mama wa vijana hao wawili yuko wapi? Watalaam wa Biblia wanadai kwamba kwa vile Simulizi la Yesu linahusu Sheria ya mirathi ambayo inasimamiwa na wanaume na inawahusu wanaume, ndiyo maana Yesu kwa makusudi mazima hakumtaja Mama watoto ili wasikilizaji walenge yale aliyokusudia Yesu kuwafundisha katika Simulizi hili - hasa Uso wa Huruma wa Baba yake wa Mbinguni!

2. Baba Anatoka Nyumbani Mara Mbili

Tumtazame kwa karibu Baba wa vijana hao wawili. Baba ambaye huruma yake inavuka mipaka yote ya ufahamu na uelewa wa kibinadamu! Ni vigumu katika mila na desturi za makabila mengi duniani kumwona baba akiamua kuacha msimamo wake wa haki na kufungua moyo na njia kwa mwana mpotevu aliyefanya madudu katika maisha yake na kutapanya mali yake. Akina baba wangapi wanamkataa na hata kumlaani kijana wa namna hii? Wangapi wanatamka wazi kwamba hawataki kumwona na wala asikanyage nyumbani tena na asithubutu hata kufika kwenye kaburi lake? Wengi tu! Lakini Baba anatoka nje mara mbili kuwatafuta wanae wote wawili na kukutana nao na kuwashirikisha huruma yake. Na japo kwa kawaida tunamwaza na kumtazama na kumlaumu zaidi bwana mdogo, lakini kusema ukweli - katika Simulizi la Yesu na katika mafundisho yake - mwenye matatazo makubwa kabisa ni kijana mkubwa. Hali yake ni mbaya sana.

Kijana huyo yuko katika hali inayofanana kabisa na hali ya Adamu baada ya kutenda dhambi ya asili. Yuko peke yake katika ulimwengu wa lawama, chuki na tuhuma. Kila mtu ni mbaya kasoro yeye. Baba ni mbaya – tena anamlaumu sana na wala hamwiti Baba hata mara moja. Si jambo la kushangaza maana tayari katika fikra zake Baba amekwishakufa na yule aliye naye nyumbani labda ni mzigo na wala hakuna uhusiano wa upendo wa kimwana kwa Mzee huyo. Hata kwa upande wa mdogo wake - huyo si mdogo wake tena - ‘na huyu mwana wako’. Katika sentensi hii fupi kijana mkubwa anajitenga na Baba na mdogo wake kwa pigo moja! ‘Na huyu mwana wako’ . Mzee ni mbaya, malezi yamemshinda, kwa sababu mtoto wake kawa mhuni na mtapanya mali.

Katika fikra za kijana mkubwa ni yeye tu yuko poa. Wengine wote - hovyo. Tena hana habari nao wala uhusiano wa kifamilia. Kijana mkubwa anahitaji wongovu wa kina, wa ndani kabisa. Ni kazi kweli kweli kwa Baba yake mwenye huruma. Baba ambaye kijana huyo hamtambui kama Baba… Baba hashindwi kazi. Huruma yake iliyojaa kabisa ndani ya nafsi yake humsukuma atoke nje awatafute wanaye na kuwaleta nyumbani wawe salama, wafufuke na kufufua upendo katika mahusiano yao ya kimwana na Baba yao.

3. Kijana Aliyekuwa Amekufa, Yu Hai.

Tumtazame na bwana mdogo, athari ya kuua uhusiano wake wa kimwana na Baba yake na uamuzi wake wa kujitenga na Baba na nyumba yao ya kifamilia. Simulizi linaeleza wazi tena kwa msisitizo kwamba kadiri bwana mdogo alivyozidi kusafiri mbali na nyumba ya Baba yake, hali ilizidi kuwa mbaya zaidi na zaidi. Alitoka nje yaNchi Takatifu na kufikia mahali ambapo watu walikuwa wanachunga na kulisha nguruwe, wanyama haramu na najisi kwa Wayahudi. Kitendo cha kuomba kazi ya kutunza nguruwe ni udhalalishaji wa hali ya juu kabisa kwa Myahudi. Na kijana alilazimika kufanya kazi hiyo kiasi kwamba alifikia hali duni kabisa ya kukosa hata chakula walichokula nguruwe! Tazameni na jaribuni kuelewa uzito na ukubwa wa anguko la kijana huyo. Jiwekeni katika nafsi yake. Safari ya dhambi ilimfikisha wapi na akajikuta katika hali gani? Hapo bwana mdogo anaanza kupata akili timamu na kwa ajili ya hali yake mbaya kabisa anaanza kukumbuka nyumbani kwao na jinsi watumishi wanavyoshiba na wana maisha mazuri tu. Njaa inamsukuma aamue kurudi nyumbani. Aibu aliyo nayo inaamsha hisia za majuto kwa Mungu na kwa Baba yake. Anaanza safari ya kuelekea nyumbani.

Hatuambiwi katika Simulizi letu hili bwana mdogo alikuwa na hisia gani wakati alipokutana na Baba yake na kuonja huruma ya pekee ya Baba ambayo kwa kweli hakustahili hata kidogo. Hatujui. Baba hampi hata nafasi ya kueleza yale aliyopanga kichwani kumshirikisha! Amerudi nyumbani kama mgeni, ombaomba, ”jobless” atafutaye kibarua. Akakutana na Baba anayefufua ndani mwake sura ya kimwana, anamrudishia hadhi yake ya kuwa mwanaye, na kufufua uhusiano wa mtoto na Baba yake! Na wakati huo Baba hata hafanyi hesabu ya gharama ya hatua alizoamua. Pesa, gharama, mchemko nyumbani na jikoni - vyote hivi si muhimu mbele ya furaha ya kufufua sura ya mtoto na hadhi yake katika kijana huyo aliyepigika vibaya sana. Kinachomfanya kijana apate uhai mpya, afufuke kama kiumbe kipya, apokelewe upya katika familia, arudishiwe heshima yake ya mtoto wa Baba - si majuto yake bali huruma isiyo na mipaka ya Babaye! Huruma ya Baba si hisia inayopita - ni hulka yake, ni matendo yake, ni tabia, ni msimamo, ni utashi wake utendao kazi ya kuleta uzima palipo na mauti…

4. “Huyu Mwana Wako” (Lk 15:32)

Katika Maandiko Matakatifu mara kadhaa tunaweza kuona kwamba kifungua mimba (firstborn) ambaye kwa kawaida, kisheria ni mrithi na mwana wa ahadi, anapata shida katika maisha yake na mahusiano yake na baba yake na kunyimwa haki zake hizo za kisheria. Tunaona hayo katika maisha ya Abeli na Kaini, Yakobo na Esau, watoto wa Yakobo na Yosefu mpaka watoto wa Yesu na Daudi. Ni jambo la ajabu kwamba sheria ya kimungu ya urithi na ahadi kwa kifungua mimba huvunjwa na Mungu mwenyewe katika kesi hizo. Na sababu ya ukiukwaji huo wa sheria unaofanywa na Mungu ni muhimu sana - katika ulimwengu wa sheria ya Mungu ya ahadi na urithi kila kitu kinatakiwa kuwekwa chini ya sheria ya Neema ya Mungu na si sheria ya kibinadamu.

Katika Simulizi letu la leo, Baba anatambua kwamba urithi unamwangukia kijana wake mkubwa, lakini pamoja na hayo anamtaka atambue hilo na kubadilisha fikra, mtazamo na mategemeo yake. Sehemu ya pili ya Simulizi tunaweza kuona kama Simulizi ndani ya Simulizi na mhusika mkuu wa sehemu hiyo ni kijana mkubwa mwenyewe. Anaporudi kutoka kazini, anakutana na sauti za machezo na muziki. Kuandaa sherehe kubwa kama hii kawaida huchukua muda. Kumbe, kijana mkubwa alifanya kazi muda mrefu na sasa katika hali ya uchovu anarudi nyumbani. Mbaya zaidi, mtumishi fulani anachochea mafuta kwenye moto wa mshangao na hasira ya bwana mkubwa akimpasha habari ya mdogo wake kurudi nyumbani na aliyoyafanya Baba yake.

Bwana mkubwa anageuka mbogo na kichaa, hasira yake haikaliki. Jamaa hashikiki! Katika hasira hiyo kali, anamshambulia Baba kwa tuhuma za ajabu na mashataka. Tofauti na Baba aliyejaa huruma kwa kijana mdogo, bwana mkubwa amejaa hasira inayomfanya apofuke asiweze kuona mambo mema yaliyotendeka katika familia yake - bwana mdogo karudi, alikuwa amepotea na kupigika lakini alirejea salama, yu mzima, na kuna kila sababu ya kumshukuru Mungu na kufurahi. Hilo jamaa haoni, wala hamwoni katika mwana mpotevu mdogo wake, anaona tu madhambi yake basi. Hivyo hawezi kuelewa na kukubali na kuthamini huruma ya Baba, wema wake na msamaha wake na furaha na upendo na hatua zote zitokanazo na huruma hiyo. Ni fujo, matusi, madharau na vurumai tu. Na kukataa kabisa kuwa sehemu ya furaha hiyo. Anakataa kata kata kujihusisha na huruma ya Baba.

Tazameni kwamba Baba hata mara moja hakueleza mwanaye mdogo alipoteza sehemu yake urithi kwa mambo mabaya gani. Ni kaka yake tu ndiye mwendesha mashtaka hodari na kubomoa wazi maovu yote ya mdogo wake - akisema kwamba kwa maisha ya uasherati na kutapanya mali na makahaba. Hapo anafanana na mwandishi wa Kitabu cha Yoshua bin Sira aliyesema: “Usiwape Malaya uhai wako, usije ukapotewa na urithi wako”. (YbS (9:6)Tunapata wasiwasi tukisoma sehemu hii ya pili ya Simulizi la Yesu. Hatima ya kijana mkubwa ilikuwaje? Alikubali kuingia na kupatana na Baba yake na kukumbatiana na mdogo wake na kumsamehe na kumpenda tena? Moyo wake ulipona? Fikra na mtazamo wake vilibadilika? Ama alizira na kuamua kuondoka nyumbani? Hatupati majibu hapa. Kwa nini?

Kwa sababu majibu tunapata katika maisha yetu, mahusiano yetu na maamuzi yetu. Simulizi la Yesu linatuachia uhuru wa kuandika mwisho wake katika maisha yetu sisi wenyewe. Je, tutaandika mwisho wa Simulizi kwa kufuata sheria za mirathi na kufuata na kudai haki? Au wataandika kwa kufuata njia ya Neema, Huruma na Msamaha? Tunaachiwa changamoto kujipima na kujitazama katika kioo cha Simulizi hili na kuona uhusiano wetu na Mungu (Baba katika Simulizi hili) ukoje? Na uhusiano wetu na jirani (bwana mdogo) ukoje?

5. Watumishi, Na Si Mahakimu, Wa Huruma

Siku hizi watalaam wengi wa Maandiko Matakatifu na wachambuzi wa Simulizi hili la Baba wa Huruma, wanachunguza kwa karibu zaidi mwenendo, misimamo, mitazamo na matamshi ya watumishi wa nyumba ya Baba. Watu hao ni sehemu muhimu na hai katika historia inayosimuliwa na kutendeka katika Simulizi letu. Tutagundua kwamba kuna makundi mawili ya watumishi hao. Kwa upande mmoja, baadhi yao wanashiriki kimatendo katika Huruma ya Baba na katika muungano wa Baba na mwana mpotevu kwa kuandaa mavazi, pete na kuandaa sherehe - chakula, muziki, mahali na kadhalika. Wanatekeleza maagizo yote bila kupingwa wakijua kinachoendelea na kwamba wanashiriki katika furaha ya Baba aliyempata kijana wake aliyekuwa amekufa na sasa yu hai na amerudishiwa hadhi na heshima yakuwa mwanaye mpendwa na mwanafamilia hai.

Ni vema tukumbuke kwamba Baba hakufanya kitu chochote katika mchakato huo – baada ya kukutana na mwanaye na kukumbatiana na kumbusu na kueleza furaha yake na huruma yake, aliwaachia watumishi uetekelezaji wa huruma yake hiyo. Baba anawashirikisha kwa makusudi mazima watumishi wake wote katika matendo ya huruma yake.  Kwa upande mwingine, tunamwona mtumishi ambaye kijana mkubwa anakutana naye baada ya kurudi nyumbani kutoka shamba na kumuuliza habari za nyumbani. Mtumishi huyo hakuwa na kauli njema sana na jinsi alivyoeleza yaliyotukia yanaashirikia kwamba alikuwa na mtazamo kama wa hakimu.

Jibu lake kwa bwana mkubwa linagusia hisia za kijana mkubwa kutotendewa haki na baba. Anaeleza tu hali ya usalama wa kimwili wa mdogo wake na kitendo cha kuchinja ndama kwa sababu ya kumpata mdogo wake tena. Mtumishi huyo hazungumzii kabisa huruma ya Baba. Jibu lake linatokana na mtazamo wake uliojikita katika sheria ya mirathi, haki na fidia ya haki. Katika mtazamo huo hakuna nafasi wala uelewa wa huruma na upendo wenye huruma. Mtumishi huyo alijua fika kwamba bwana mkubwa hajawahi kuchinjiwa hata mbuzi na Baba yake. Na wakati huu mwana mpotevu anachinjiwa ndama iliyonona, iliyo bora. Kwa nia ya kumuumiza na kumchokoza anamwambia - “Tazama, uaminifu wako na kazi ngumu unayofanya vizuri kwa miaka yote machoni pa Baba yako havistahili hata mbuzi; na wakati huo maisha ya hovyo, ya ufuska na ya kihuni ya mdogo wako machoni pa Baba yako yanafaa kuchinjiwa ndama bora!”

Maneno ya mtumishi yanageuka kuwa kiberiti katika kituo cha mafuta. Bwana mkubwa analipuka hasira na yatokanayo na vurumai hizo tunaona katika Simulizi. Kwa kifupi, kwa kutazama na kutafakari nafasi ya watumishi katika Simulizi hili la Yesu, tunaweza kusema kwamba baadhi yako ni watumishi wa Huruma wanaoshirikiana kutekeleza Huruma ya Baba kwa mwanaye mpotevu na kumrudisha katika hadhi ya kuwa mwana hai na mrithi. Na baadhi yao ni Mahakimu wanaomtuhumu Baba kwa Huruma yake inayozidi mipaka na kuwakwaza watu.

Na Padre Wojciech Adam Koscielniak

Kituo cha Hija Kiabakari, Jimbo Katoliki Musoma.








All the contents on this site are copyrighted ©.