2016-03-08 10:30:00

Hata shule za kata zinaweza kuunda "Magenius"!


Waziri mkuu wa Tanzania Kassim Majaliwa amesema shule za sekondari za kata zina fursa ya kufanya vizuri kama zilivyo shule nyingine licha ya kuwa watu wengi wamekuwa wakizidharau. Ametoa kauli hiyo Jumatatu, Machi 7, 2016 wakati akikabidhi zawadi ya kompyuta mpakato (laptop) kwa mwanafunzi aliyeshinda shindano la kuandika insha katika nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC ). Kompyuta hiyo ina thamani ya sh. 1,992,000/-.

Mwanafunzi huyo, Jabir Mandando (20), amehitimu kidato cha nne katika shule ya sekondari ya Mbekenyera iliyoko wilayani Ruangwa mkoani Lindi. Amepata ufaulu wa daraja la pili na sasa anasubiri matokeo ya kujiunga na kidato cha tano. Lakini aliandika insha hiyo mwaka jana wakati akiwa kidato cha nne. "Huyu ni mtoto wa kijijini tu. Anatoka kijiji cha Namilema wilaya ya Ruangwa mkoa wa Lindi. Shule ya Mbekenyera aliyosoma ni shule ya kata. Ameweza kushinda tuzo na kushika nafasi ya tatu katika shindano lililoshirikisha shule nyingi za Jumuiya ya Afrika Mashariki."

"Jabir ameweza kuchomoza kitaifa kwa kushiriki shindano la kimataifa. Nimeamua kumpa zawadi ya laptop pamoja na begi lake ili aweze kujisomea zaidi na kupata elimu ya masuala mbalimbali kwa kutumia kompyuta hii. Pia nataka iwe ni chachu kwa vijana wengine kushiriki mashindano kama haya," alisema Waziri Mkuu. Waziri Mkuu pia alikabidhi Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Bw. Shanael Nchimbi fedha taslimu sh. 500,000/- zikiwa ni zawadi kwa ajili ya shule hiyo. mwalimu Nchimbi alimsindikiza mwanafunzi huyo Arusha kupokea zawadi hizo kwenye mkutano wa Wakuu wa Nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki uliomalizika Arusha wiki iliyopita.

Kwa upande wake, kijana Jabir alisema anashukuru sana kwa zawadi aliyopewa na kuahidi kuwa atajitahidi kusoma kwa bidii masomo ya kidato cha tano na sita ili aweze kutimiza ndoto yake ya kuwa daktari. Alipoulizwa alipataje taarifa ya uwepo wa shindano hilo, Jabir alisema: "Walimu walipata taarifa wakazileta darasani na kutuambia tushiriki kuandika. Walizikusanya na kuchagua tatu bora, ndipo yangu ikashinda." Amesema insha aliyoiandika ilihusu: "The importance of political stability in the East African Integration."  Alimwonyesha Waziri Mkuu cheti na dola za Marekani 200 ambavyo alipewa zawadi kutokana na ushindi huo. Shule ya Mbekenyera ambayo alikuwa akisoma, pia ilizawadiwa laptop na printer kutokana na ushindi wa kijana Jabir.

Mshindi wa kwanza katika shindano hilo ametoka shule ya Sekondari Mzumbe, mshindi wa pili alitoka Kenya na wa tatu alitoka shule ya Mbekenyera.

Na Ofisi ya Waziri mkuu wa Tanzania.








All the contents on this site are copyrighted ©.