2016-03-07 10:47:00

Watoto wa kike millioni kumi na sita, hawana fursa ya masomo!


Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni la Umoja wa Mataifa, UNESCO katika taarifa yake linaonesha kwamba, duniani kuna watoto wa kike zaidi ya millioni kumi na sita, kati ya umri wa miaka 6 hadi 11 ambao hawatapata kamwe fursa ya kuingia darasani ili kupata elimu ya awali itakayowasaidia kuwa na  matumaini kwa siku za usoni ikilinganishwa na watoto wa kiume. Hii ina maana kwamba, mkazo mkubwa wa elimu unatolewa kwa watoto wa kiume, ikilinganishwa na watoto wa kike wanaoendelea kubakizwa nyumba kama “mkia wa kondoo”.

Taarifa ya UNESCO ni sehemu ya maandalizi ya maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani inayoadhimishwa na Jumuiya ya Kimataifa kila mwaka ifikapo tarehe 8 Machi. Watoto wa kike wananyimwa haki yao msingi ya kupata elimu ya awali ili kujijengea matumaini ya maisha bora zaidi kwa siku za usoni. Watoto wa kike wameathirika zaidi na ujinga huko Asia ambako asilimia 80% ya watoto wa kike hawapati nafasi ya kwenda shule. Hapa UNESCO inasema, kuna haja ya kufanya mageuzi ili kubadilisha mwelekeo huu, kwa kutoa kipaumbele cha pekee kwa watoto wa kike ili waweze kupata fursa ya kwenda shule!

Ukosefu wa usawa wa elimu kutokana na jinsia unashuhudiwa pia Barani Afrika, Kusini mwa Jangwa la Sahara na katika baadhi ya Nchi za Kiarabu. Kwa mwelekeo hasi namna hii, itakuwa ni vigumu kwa Jumuiya ya Kimataifa kufanikisha Lengo la Maendeleo endelevu ifikapo mwaka 2030, ikiwa kama umaskini, ujinga na maradhi yataendelea kuwasonga watoto wa kike kwa vile tu hawakupata fursa ya kwenda shule! Hapa kuna haja kwa Jumuiya ya Kimataifa kujifunga kibwebwe ili kupambana na ubaguzi na umaskini unaoendelea kuwaandama wanawake na watoto wa kike, anasema Bi Irina Bokova, Mkurugenzi mkuu wa UNESCO.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.