2016-03-07 08:17:00

Siku ya Wanawake Duniani "50 - 50 Ifikapo 2030; Tuongeze Jitihada"


Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na watoto inawataarifu wananchi wote kuwa tarehe 8 Machi ya kila mwaka Tanzania huungana na nchi nyingine wanachama wa Umoja wa Mataifa kuadhimisha Siku ya Wanawake Duniani.  Maadhimisho ya Siku ya Wanawake, hutoa fursa kwa Serikali, wananchi, wadau, na wanawake wenyewe kupima utekelezaji wa maazimio, matamko na mikataba ya Kimataifa, Kikanda na Kitaifa inayohusu masuala ya maendeleo ya wanawake na usawa wa jinsia.

Siku ya wanawake Duniani husisitiza kujenga mshikamano wa wanawake wote duniani, kuhamasisha jamii kutafakari kaulimbiu ya Maadhimisho ya Siku ya Wanawake ya kila mwaka; kuelimisha jamii kuhusu jitihada mbalimbali zilizofanywa na Serikali na asasi mbalimbali yakiwemo Mashirika Yasiyo ya Kiserikali katika kuwaendeleza wanawake; na kuhamasisha jamii kuhusu utekelezaji wa sera na mipango mbalimbali ya Serikali yenye lengo la kudumisha Amani, Usawa na Maendeleo.

Kaulimbiu ya kitaifa ya Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani mwaka 2016 inasema “50– 50 Ifikapo 2030; Tuongeze Jitihada”. Kaulimbiu hii inasisitiza kuwa na mikakati thabiti yenye mwelekeo wa kufikia Agenda 2030 ya malengo inayohimiza kufikia asilimia 50 kwa 50 ya ushiriki wa wanawake na wasichana katika nyanja zote za maendeleo.

Kuanzia mwaka 2005 Serikali ilipitisha uamuzi kuwa, maadhimisho haya yafanyike Kitaifa kila baada ya miaka mitano kutoa muda wa utekelezaji wa maazimio na kupima mafanikio yaliyofikiwa katika kipindi cha miaka mitano. Mwaka 2015 Maadhimisho yalifanyika Kitaifa mkoani wa Morogoro. Kwa mwaka 2016, mikoa yote itaadhimisha siku hii katika maeneo yao kwa kuzingatia hali na mazingira ya mikoa husika. Kwa mfano mkoa wa Dar es salaam, utaadhimisha siku hii katika Manispaa ya Kinondoni. Wizara inatoa wito kwa mikoa yote kuhamasisha wananchi na wadau wote kushiriki maadhimisho ya siku hii adhimu na kuzingatia ujumbe wa kauli mbiu ya mwaka 2016.

Rai yangu kwa wadau wote ni kuwa, tuunge mkono jitihada za Serikali katika kutoa haki na ushiriki sawa katika fursa za uongozi wa kisiasa na kiuchumi; na kupima mafanikio yaliyofikiwa na kuweka mipango yenye matokeo makubwa, na kubainisha shuhuda za wanawake waliotoa mchango uliotukuka katika kuwezesha maendeleo ya wanawake wenywe na taifa kwa ujumla. Nashauri wanahabari wote kuelimisha jamii kuhusu kaulimbiu ya Siku ya Wanawake kwa mwaka 2016 ili kila mwananchi aweze kutambua jukumu alionalo katika kufikia lengo la ushiriki sawa wa wanawake na wasichana katika uchumi; afya, elimu, ajira, sheria na siasa ifikapo mwaka 2030. Nawatakia mafanikio mema katika maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani mwaka huu.

Sihaba Nkinga

KATIBU MKUU








All the contents on this site are copyrighted ©.