2016-03-07 14:44:00

Hili ni wiki ya mafungo ya kwaresima kwa Papa na wasaidizi wake


Kwa muda wa wiki nzima, Baba Mtakatifu Francisko na wasaidizi wake katika  idara za Curia ya Roma,  tangu Jumapili 6 Machi 2016 jioni walianza mafungo ya Kiroho ya Kwaresima. Hivyo  Papa amefuta  shughuli zote za kukutana na watu mbalimbali, ikiwemo katekesi yake ya Jumatano kwa mahujaji na wageni.  Papa anafanya mafungo haya akiwa katika kituo cha Kiroho cha Casa del Divin Maestro” cha Ariccia , kilicho nje kidogo ya Jiji la Roma , umbali wa kilomita 25. Padre  Ernest Ronchi, Mtawa wa Shirika la Watumishi wa Bikira Maria ataongoza tafakari za mafungo hayo yanayokamilika  Siku ya Ijumaa  11 Machi kwa  Ibada ya Misa na kuabudu Ekaristi.  Taarifa inasema  Mandhari ya Mafungo ya Papa na wasaidizi wake, inaongozwa baadhi ya maswali ya Yesu kwa wafuasi wake yaliyomo katika vitabu vinne vya Injili.

Padre Ernesti Ronchi, Jumapili jioni, akizindua kipindi hiki cha mafungo, alilenga  katika swali la Yesu kama ilivyoandikwa katika kitabu cha Injili Yohana ambamo  "Yesu aliwauliza wanafunzi„ "Mnatafuta nini".

 Katika maelezo yake, Padre Ronchi alisema,  hata leo Yesu  anauliza wafuasi wake "Mnamtafuta nani". Hoja inayodai kumsikiliza Mungu anayewahoji na kutoa jibu , na si wao kumhoji   Mungu, ili mwachie Yeye awahoji.  Alionya dhidi ya kukimbilia kutoa jibu kwa  harakaharaka aksiema ni lazima kwanza kusikiliza kwa makini swali na ndipo kutoa  jibu kutoka kina cha moyo, jibu linalofaa  kuendesha maisha.  Na kwamba , maswali yote yaliyoulizwa na Yesu ni maswali  mazuri yanayotafuta kuitajirisha roho kwa imani na yanaonyesha uwazi wa Injili katika maisha.  Na kwamba kupenda kusikiliza maswali kwa makini, huku tayari ni kutafuta kufunuliwa .  Kusikiliza kwa makini swali, huonyesha  uongofu.

Padre Ronchi aliendelea,  kiimani  kuwa tayari kujielimisha kwa njia ya kujibu maswali, kunafaa zaidi ya  njia kutumia  maneno  matupu. Na kwamba katika vitabu vinne vya Injili , mna maswali  zaidi ya 220 yaliyoulizwa na Yesu. Aulizaye swali maana yake ,  anataka kujua zaidi hivyo maswali  ni  njia ya  mawasiliano na si upinzani au vurugu za kutaka kumshambulia mwingine, na kwa kawaida, maswali  huongoza  katika mwanzo wa mazungumzo, au mwanzo wa kushirikishana mawazo,  kila mmoja akitoa maoni yake kwa uhuru kamili.  Kwa Maana hiyo Yesu mwenyewe anakuwa swali kwetu. Maisha yake na kifo chake vinakuwa changamoto inayowataka waamini, watoe jibu katika swali  nini  maana mwisho wa maisha , na wanapaswa kufanya nini kwa ajili ya kuwa  maisha ya furaha.  Jibu la swali hilo, bado ni  kwake  Yesu.

Padre Rochi aliendelea kuzungumza  maisha ya Furaha ya kuwa na Yesu , akisema , zaidi ya yote ni maisha ya uchaji na unyenyekevu wa kujirudi kiroho ili kupata kuelewa   kile  kinachohitajika zaidi katika kuyapata maisha ya furaha.  Na kuitafuta  furaha ni kumtafuta Mungu ambaye hupatikana katika vyote, mazuri na  hata katika "mateso”, kwa kuwa katika mateso pia tunaweza kugundua  uzuri wa kuishi na  Kristo, kama historia yake inavyotuonyesha. Yeye ni habari njema , inayoweza kumfkia  kila mmoja na  kuwa na maisha mazuri kama mtu binafsi au jamii kwa ujumla.  

Padre Ronchi amehimiza  kuendelea kumtafuta Mungu kwa moyo wote, kwa kuwa ni Yeye anayeleta furaha kamili moyoni, na ni Yeye  ambaye jina lake pia  ni furaha, uhuru na ukamilifu.  Na ni kazi ya waamini kutangaza uzuri wa Mungu , kama ndiye  hitaji la  kuvutia.  Wakati huohuo Padre Ronchi pia  alionya juu ya udhaifu wa binadamu  kwamba isiwe kizuizi katika kutangaza uzuri wa Mungu, kwa kuwa bindamu wote wameumbwa na asili hii ya udhaifu wa kutenda dhambi lakini Mungu ni mwenye huruma nyingi,  anajua udhaifu huo na hivyo hachoki kumpokea  kila anayepiga magoti mbele yake na kumwabudu.    Kila mmoja basi, na atambue udhaifu wake na kufanya toba na kumrejea Mungu kwa kuongozwa na mwanga  wa maonjo , mtazamo na hamu  zote za kumtafuta Mungu .  Kila mmoja anahitaji kunywa kutoka katika kisima cha mwanga usiokuwa na mipaka. Daima tunahitaji kusikiliza swali analouliza Yesu hata kwa wakati huu,  Mnamtafuta nani? Kwa nani mnakwenda? Jibu letu na litoke ndani ya kina cha moyo kwamba, ”  Ninamtafuta Mungu, nina hamu ya kwenda kwake  yeye mwenye kuuufanya moyo kuwa na furaha kamili. 








All the contents on this site are copyrighted ©.