2016-03-05 11:49:00

Papa asikitishwa na mauaji ya watawa huko Yemen!


Baba Mtakatifu Francisko amepokea kwa uchungu na masikitiko makubwa taarifa ya mauaji ya kinyama yaliyofanywa na kikundi cha kigaidi dhidi ya watawa wanne wa Shirika la Wamissionari wa upendo, maarufu kama Watawa wa Mama Theresa wa Calcutta waliokuwa wanafanya kazi na utume wao mjini Aden, Yemen. Kuna watu wengine kumi na wawili wameuwawa pia katika shambulio hili la kigaidi.

Baba Mtakatifu katika ujumbe ulioandikwa kwa niaba yake na Kardinali Pietro Parolin anapenda kuwahakikishia wote walioguswa na mashambulizi haya uwepo wake wa karibu. Anaendelea kusali ili mauaji haya yasaidie kuamsha dhamiri na hatimaye, toba na wongofu wa ndani, ili kuweka silaha chini na kuanza mchakato wa kutafuta amani kwa njia ya majadiliano.

Baba Mtakatifu anawaalika wahusika wakuu katika vita hii kuweka silaha zao chini, ili kuwasaidia wananchi wa Yemen, hasa wale maskini, ambao watawa hawa walijisadaka kwa ajili ya kuwahudumia kwa upendo na ukarimu. Baba Mtakatifu anawaombea wote walioguswa na mashambulizi haya baraka na anapenda kuonesha mshikamano wake wa dhati na Wamissionari wote wa upendo kutokana na msiba huu mzito!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican. 








All the contents on this site are copyrighted ©.