2016-03-05 16:34:00

Mwaka wa huruma ya Mungu uwasaidie watu kuamini zaidi!


Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican kunako tarehe 8 Desemba 1965 walihitimisha maadhimisho ya Mtaguso na huo ukawa ni ukurasa mpya wa maisha na utume wa Kanisa linalosafiri na walimwengu katika raha, shida na matumaini yake, Kanisa ambalo ni kwa ajili ya watu pamoja na watu, ili liweze kuwapeleka kwa Mwenyezi Mungu kwa njia ya Kristo Yesu. Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican ilikuwa ni zawadi kubwa kwa Kanisa katika mapambazuko ya Millenia ya tatu ya Ukristo na chachu ya ari na mwamko mpya wa missionari ndani ya Kanisa.

Changamoto kubwa kwa sasa, Mama Kanisa anapoadhimisha kumbu kumbu ya Jubilei ya Miaka 50 tangu kuhitimishwa kwa maadhimisho ya Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican ni kuhakikisha kwamba, mambo msingi yaliyoamriwa na Mababa wa Mtaguso yanafanyiwa kazi katika maisha na utume wa Kanisa. Kwa namna ya pekee anaasema Kardinali Philippe Barbarin katika Waraka wake wa kichungaji kwa ajili ya maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei kuu ya huruma ya Mungu, waamini wanapaswa kuonesha na kushuhudia huruma na upendo wa Mungu katika maisha yao na kwa jirani zao.

Ni mwaliko wa kutoka na kuwaendelea wengine, changamoto hai inayotolewa na Baba Mtakatifu Francisko kwa Kanisa la nyakati hizi. Barua hii ya kichungaji imesambazwa kwa waamini wote wa Jimbo kuu la Lione, nchini Ufaransa ili iwasaidie kuishi kikamilifu Mwaka mtakatifu wa huruma ya Mungu. Katika maadhimisho ya Mwaka huu, kila Parokia inaalikwa kuibua mpango wa kimissionari utakaofanyiwa kazi katika kipindi chote cha maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei kuu ya huruma ya Mungu, ili kweli mwaka huu uweze kuacha chapa ya kudumu katika maisha na miyo ya waamini wanaosafri hapa duniani.

Hiki ni kipindi pia cha Uinjilishaji mpya na Katekesi ya kina changamoto iliyotolewa na Mwenyeheri Paulo wa VI katika Waraka wake wa kitume Evangelii nuntiandi; Mtakatifu Yohane Paulo II katika Waraka wake wa Redemptoris missio unaohusu utume wa Kimissionari na wakati huu Baba Mtakatifu Francisko anapowahamasisha waamini kujikita katika utangazaji na ushuhuda wa Injili ya furaha, Evangelii gaudium.

Hizi ni nyaraka muhimu sana kwa maisha na utume wa Kanisa kama sehemu ya mchakato endelevu wa kukazia katekesi makini inayojikita katika: Imani, Sakramenti za Kanisa, Maisha adili na Sala; mambo yanayomwilishwa katika ushuhuda wa imani tendaji, changamoto kubwa katika Uinjilishaji mpya. Kardinali Barbarin anakaza kusema kama Mtakatifu Paulo, Ole wangu ikiwa kama nitashindwa kuhubiri Injili! Lakini mahubiri haya yanapaswa kujikita katika maneno na kushuhudiwa kwa njia ya imani tendaji! Watu wanataka kuona matendo, wamechoka kusikia “ngebe za watu”.

Jumuiya za Kikristo zinaweza kuwa ni chachu ya ari na mwamko mpya wa kimissionari ikiwa kama zitajikita katika ujenzi wa udugu, umoja na mshikamano wa dhati kwa kutambua kwamba, Kanisa ni mhudumu wa Mafumbo matakatifu n ani chombo cha umoja, mshikamano, imani na mapendo. Kanisa katika Mafundisho yake tanzu, linalotoa na kushuhudia mwanga wa imani inayobubujika kutoka kwa Krisyo kwa ajili ya watu wake. Kanisa katika ulimwengu mamboleo linahamasishwa kuwa ni mhudumu wa mahitaji msingi ya binadamu. Ili kuwa kweli na mradi wa kimissionari, Neno la Mungu, Sakramenti za Kanisa, Maisha ya Adili na Maisha ya Sala ni mambo ambayo yanapaswa kupewa kipaumbele cha pekee katika maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei kuu ya huruma ya Mungu.

Neno la Mungu liwe ni chachu ya ujenzi wa Jumuiya ya Kikristo inayoboreshwa kwa maisha ya Kisakarmenti na kujikita katika ushuhuda wa maisha adili na sala, kielelezo cha imani tendaji. Waamini wajenge na kudumisha utamaduni wa kusali, kutafakari na kumwilisha Neno la Mungu kwa njia ya matendo ya huruma: kiroho na kimwili; mambo msingi wakati huu wa maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei kuu ya huruma ya Mungu anasema Kardinali Philippe Barbarin, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Lione, Ufaransa, katika Waraka wake wa kichungaji wakati huu wa maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei kuu ya huruma ya Mungu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican. 








All the contents on this site are copyrighted ©.