2016-03-05 08:10:00

Mashuhuda wa huruma ya Mungu, wauwawa kikatili nchini Yemeni


Kardinali Oswald Gracias, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki India anasema, Kanisa na wapenda amani duniani wamesikitishwa sana na mauaji ya kikatili waliyotendewa Watawa wanne wa Shirika la Wamissionari wa Upendo, maarufu kama Masista wa Mama Theresa wa Calcutta, waliouwa mjini Aden, nchini Yemeni wakati wakitoa huduma kwenye nyumba ya wazee, Ijumaa tarehe 4 Machi 2016. Taarifa za ulinzi na usalama nchini Yemeni zinasema, mashambulizi haya yamefanywa na vikundi vya kigaidi nchini humo!

Kati ya watawa wawili wanatoka Rwanda, Kenya na India. Mama mkuu wa Jumuiya ameponea chupuchupu kuuawa na magaidi hao. Inasikitisha kuona kwamba, watawa hawa ambao wamejipambanua kama vyombo na mashuhuda wa huruma ya Mungu kwa maskini, wanauwawa kikatiliki kiasi hiki, wakati wa maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu, ambamo waamini wanaalikwa kwa namna ya pekee kumwilisha matendo ya huruma kiroho na kimwili katika uhalisia wa maisha ya watu!

Kardinali Oswald Gracias anasema, Wamissionari wa Mama Theresa wa Calcutta wamekuwa mstari wam bele kuzima kiu ya Yesu kwa kuwasaidia na kuwahudumia wazee na wagonjwa nchini Yemeni. Wamewaonesha moyo wa upendo, huruma, ukarimu na utu wema, hata pale usalama wa maisha yao ulionekana kuwa hatarini zaidi, lakini wakaendelea kutoa huduma kwa maskini na wale wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii.

Hawa ni mashuhuda wa huduma ya upendo kwa Kristo Yesu inayojionesha kwa namna ya pekee kabisa kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Ni matumaini ya Kardinali Gracias kwamba, damu ya watawa hawa itakuwa kweli ni mbegu ya matunda ya amani kwa ajili ya wananchi wa Yemen ambao kwa sasa wanakabiliwa na hali tete sana ya maisha kutokana na mashambulizi ya kigaidi yanayoendelea kutishia usalama, amani na utulivu.

Kardinali Oswald Gracias anamkumbuka na kumwombea Padre Tom Uzhunnalil kutoka Shirika la Wasalesiani wa Don Bosco ambaye alikuwa anatekeleza utume wake mjini Aden, hadi sasa hajulikani mahali alipo! Watawa hawa wamekumbukwa kwa namna ya pekee katika Ibada ya mpango mkakati wa Saa 24 kwa ajili ya Bwana, kielelezo cha mshikamano na Khalifa wa Mtakatifu Petro wakati huu wa maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.