2016-03-04 07:05:00

Ubaguzi ni ukiukwaji wa haki msingi za binadamu!


Ubaguzi wa rangi ni dhambi na uovu unaoigawa familia ya binadamu kwa kukana uumbaji mpya na ukombozi wa dunia, changamoto ya kusimama kidete ili kuhakikisha kwamba, ubaguzi unang’olewa katika akili na mioyo ya watu, ili kujenga jamii bora zaidi kwa siku za usoni. Tatizo la ukosefu wa maridhiano kati ya watu linalopelekea: mauaji, dhuluma na nyanyaso kutokana na tofauti za kidini na kikabila linapaswa kudhibitiwa kwa kutambua kwamba, wote wanaguswa na madhara haya.

Watu waonane na kutambua uwepo wa jirani zao, ili kukuza na kudumisha utu na heshima ya binadamu pamoja na utambulisho wa mtu, vinginevyo kuna hatari ya mtu kukata tamaa katika maisha ya kijamii na kisiasa na madhara yake ni makubwa sana katika medani mbali mbali za maisha ya watu! Ubaguzi wa rangi unawanyima watu mahitaji msingi kama vile: makazi bora, elimu, fursa za ajira na huduma kwa wazee; mambo ambayo pia ni ukosefu wa haki jamii.

Ubaguzi wa rangi ni mateso yanayowasumbua watu wa pande zote, wale wanaowabagua wenzao na wale wanaobaguliwa, ndiyo maana hata leo hii madhara ya biashara ya utumwa bado yanaendelea kuwatendea watu mbali mbali! Kumbe, kuna haja ya kujenga na kudumisha umoja na udugu uliokusudiwa na Mwenyezi Mungu pale alipomuumba binadamu kwa sura na mfano wake. Ubaguzi wa rangi unapaswa kung’olewa kutoka katika akili na sakafu ya mioyo ya watu.

Hii ni sehemu ya ujumbe ulioandikwa na Kardinali Peter Turkson, Rais wa Baraza la Kipapa la haki na amani katika maadhimisho ya mkutano unaojadili kuhusu ubaguzi wa rangi huko Birmingham, Alabama, Marekani kuanzia tarehe 3- 4 Machi, 2016. Kardinali Turkson anawahimiza watu kujenga na kudumisha upendo unaowasaidia watu kuheshimiana na kuthaminiana kama ndugu, huku wakiwa na uwezo wa kuona utu na heshima ya binadamu aliyeumbwa na anayependwa na Mungu.

Ili kupambana na ubaguzi wa rangi, kuna haja ya kukuza na kudumisha elimu makini miongoni mwa vijana wa kizazi kipya ili kuhakikisha kwamba, ndago za ubaguzi wa rangi zinang’olewa mapema iwezekanvyo katika akili na mioyo ya watu. Mchakato huu hauna budi kwenda sanjari na uponyaji wa ndani na nje kwa wale walioathirika kutokana na ubaguzi, kwa kutambua kwamba, wote wanaunda familia moja ya binadamu.

Huu ni wakati muafaka wa kutafakari kuhusu imani mintarafu ubaguzi wa rangi kwa kuchunguza vyema dhamiri kwani dhana hii pia ni chanzo kikuu cha umaskini na uvunjaji wa haki msingi za binadamu. Binadamu wote wameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu, changamoto ya kujenga na kudumisha utamaduni wa watu kukutana, kuheshimiana na kusameheana.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.