2016-03-04 06:53:00

Timor ya Mashariki na Vatican watia sahihi itifaki ya makubaliano!


Baba Mtakatifu Francisko Alhamisi tarehe 3 Machi 2016 amekutana na kuzungumza na Bwana Rui Maria de AraĆ¹jo, Waziri mkuu wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Timor ya Mashariki pamoja na ujumbe wake waliofika mjini Vatican ili kuridhia itifaki ya ushirikiano kati ya Timor ya Mashariki na Vatican pamoja Kanisa nchini humo. Itifaki hii ilitiwa sahihi kunako tarehe 14 Agosti 2015 na hivyo kuweka kisheria mahusiano kati ya Serikali ya Timor ya Mashariki na Vatican na kati ya Kanisa Katoliki na Serikali ya Timor ya Mashariki.

Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican ameongoza ujumbe wa Vatican katika kuridhia Itifaki hii ya ushirikiano kati ya Serikali ya Timor ya Mashariki na Vatican na Bwana Aderito Hugo da Costa amewakilisha ujumbe wa Serikali ya Timor ya Mashariki. Itifaki hii itaanza kutekelezwa rasmi pale pande zote mbili zitakapokuwa zimeridhia itifaki hii.

Katika hotuba yake, Kardinali Parolin ameishukuru Serikali ya Timor ya Mashariki kwa ushirikiano wake, lakini kwa namna ya pekee alipokuwapo nchini mwao katika maadhimisho ya Jubilei ya miaka 500 ya Uinjilishaji huko Timor ya Mashariki na kwa wakati huu wanapotia sahii itifaki ya ushirikiano kati ya nchi hizi mbili. Hizi ni juhudi za majadiliano ya kina kati ya Kanisa na Serikali, ili kulisaidia Kanisa kutekeleza dhamana, wajibu na utume wake nchini humo kama sehemu ya mchakato wa kumwendeleza mtu mzima: kiroho na kimwili kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa maskini na wale wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii.

Itifaki hii ni chombo muhimu kitakacholiwezesha Kanisa kutekeleza wajibu wake kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya Familia ya Mungu Timor ya Mashariki, kwa kukazia zaidi misingi ya haki, amani, uhuru na utulivu. Kanisa litaweza kuleta maendeleo makubwa, ikiwa kama yale yaliyoandikwa kwenye itifaki hii yatapokelewa na kufanyiwa kazi!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.