2016-03-04 14:57:00

Mpango mkakati wa Saa 24 kwa ajili ya Bwana!


Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wake wa Uso wa huruma “Misericordiae vultus” anasema waamini wengi wakiwemo vijana wameanza hija ya kurudi kujipatanisha na Mungu kwa njia ya Sakramenti ya Upatanisho, ili kuimarisha zaidi maisha yao ya Kikristo kwani Sakramenti ya Upatanisho inamfanya wamini aguse kwa mkono wake ukubwa wa huruma na upendo wa Mungu, chemchemi ya furaha na amani ya ndani!

Baraza la Kipapa la Uhamasishaji wa Uinjilishaji mpya lililopewa dhamana ya kuratibu matukio ya maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu linasema, mpango mkakati wa saa 24 kwa ajili ya Bwana unaoadhimishwa na Kanisa zima kati ya tarehe 4 - 5 Machi, 2016 ni kielelezo cha mshikamano wa imani na Baba Mtakatifu Francisko, ili waamini katika umoja na mshikamano wao, waweze kuonja huruma ya Mungu katika maisha yao.

Hili ni tukio ambalo linataka kuhimiza kwa namna ya pekee umuhimu wa maisha ya sala, tafakari ya Neno la Mungu na Sakramenti za Kanisa katika maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu, ambamo mwaamini wanaalikwa kuyamwilisha yote haya katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili, kielelezo makini cha imani tendaji. Iweni na huruma kama Baba ndiyo kauli mbiu inayoongoza maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu.

Itakumbukwa kwamba, kunako mwaka 2014 siku hii iliongozwa na kauli mbiu “Msamaha una nguvu zaidi kuliko dhambi” na kunako mwaka 2015, ikaongozwa na kauli mbiu “Mungu, mwingi wa huruma”.  Malango ya Huruma ya Mungu anasema Askofu mkuu Salvatore Rino Fisichella yanapatikana walau katika kila Jimbo, lakini Roma bado ina nafasi ya pekee katika maisha na utume wa Kanisa kwani hapa ni kitovu cha imani.

Huruma ya Mungu inafumbatwa katika nyanja mbali mbali za maisha ya mwanadamu na wala si tu katika Sakramenti ya Upatanisho ingawa inapewa kipaumbele cha pekee sanjari na matendo ya huruma kiroho na kimwili katika maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu. Sala na tafakari ya Neno la Mungu ni fursa muhimu sana inayomwezesha mwamini kuvuta huruma na msamaha wa Mungu katika maisha yake. Waamini watumie fursa hii kujuta, kutubu na kuungama dhambi pamoja na kujisadaka kwa ajili ya sala na Ibada ya Kuabudu Ekaristi Takatifu. Waamini wanahamasishwa kuwashirikisha jirani zao mang’amuzi ya “Mpango mkakati wa saa 24 kwa ajili ya Bwana” kwa njia ya mitandao ya kijamii!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.