2016-03-04 07:20:00

Huruma ya Mungu!


Idara ya Toba ya Kitume ni mahali ambapo mwamini anaonja huruma na upendo wa Mungu, tayari kujipatanisha na Kristo na Kanisa lake. Hii ni kati ya idara za zamani kabisa kuanzishwa na Vatican katika maisha na utume wa Kanisa. Hii ni mahakama ya huruma ya Mungu inayopania kujenga na kudumisha uhusiano mwema kati ya mdhambi na Mungu mwingi wa huruma na mapendo.

Hivi ndivyo anavyosema Askofu mkuu Krzysztof  Nykiel hakimu wa mahakama ya huruma ya Mungu katika kozi maalum kwa ajili ya Mapadre waungamishaji wakati huu Mama Kanisa anapoadhimisha Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu kwa kutoa kipaumbele cha pekee katika toba na wongofu wa ndani pamoja na matendo ya huruma: kiroho na kimwili.

Askofu mkuu Nykiel amepembua kwa kina na mapana: miundo mbinu; dhamana na wajibu wa mahakama ya huruma ya Mungu ambayo kimsingi ina uhusiano wa karibu zaidi na utume wa Khalifa wa Mtakatifu Petro kama huduma msingi ya maisha ya kiroho kwa ajili ya wokovu wa roho za watu. Mahakama hii inasaidia mchakato wa waamini wanaotaka kujipatanisha na Mwenyezi Mungu, Kanisa na jirani zao kwa kutambua kwamba, upatanisho ulioletwa na Kristo Yesu na kwa njia ya Roho Mtakatifu unatekelezwa ndani ya Kanisa linalotekeleza dhamana na wajibu wake katika historia na nyakati, kwa kuungana na Kristo ambaye ni kichwa cha Kanisa lake.

Huu ndio ukweli ambao kwa bahati mbaya, waamini wengi wanashindwa kuumwilisha katika uhalisia wa maisha yao, kwani Kanisa linasamehe dhambi kwa niaba ya Kristo aliyetumwa na Mwenyezi Mungu duniani. Waamini watambue na kukiri uwepo wa dhambi, tayari kukimbilia huruma na upendo wa Mungu katika maisha yao. Mahakama ya huruma ya Mungu ni tofauti kabisa na utendaji wa kazi wa mahakama kama zinavyofahamika na wengi. Hii ni mahakama inayompatia mwamini nafasi ya kufafanua hali ya maisha yake kiroho, ili kuomba huruma na msamaha wa Mungu. Hapa ndipo mahali ambapo watu wenye vikwazo katika maisha, Sakramenti na utume wa Kanisa wanaweza kupata msamaha na maondoleo ya dhambi zao.

Askofu mkuu Nykiel anafafanua kwamba mahusiano ya dhati kati ya mwamini na Mwenyezi Mungu yanarejeshwa tena kwa njia ya Kanisa, ili kuweza kujipatia tena maisha ya uzima wa milele. Mwamini anajipatanisha na Mungu, Kanisa na jirani zake kwa njia ya maondoleo ya dhambi ambayo kimsingi ina madhara yake katika maisha na utume wa Kanisa. Mahakama ya huruma ya Mungu inatekeleza dhamana yake kwa usiri mkubwa wala hakuna malumbano na kwamba, hii ni taasisi ambayo inabaki ikiendelea kutekeleza dhamana na wajibu wake hata pale ambapo Kiti cha Khalifa wa Mtakatifu Petro kiko wazi kwa sababu mbali mbali.

Kuna dhambi ambazo zinaondolewa tu na Kiti kitakatifu na kwamba, mwamini yoyote anayetenda dhambi hizi anajiondoa kwenye Kanisa mara moja kwa kitaalam hali hii inajulikana kama “Latae sententiae”: yaani:  kufuru dhidi ya Ekaristi Takatifu; kutoa siri za maungamo; Padre kumwondolea mwamini dhambi ambazo wametenda pamoja kwa mfano kwa kuzini; kwa kumjeruhi Khalifa wa Mtakatifu Petro; Kwa kumweka wakfu Askofu bila kibali wala ruhusa ya Khalifa wa Mtakatifu Petro au kutoa Sakramenti ya Daraja Takatifu kwa mwanamke. Rufaa ya maondoleo ya dhambi hizi inafanyika kwa njia ya barua ambayo ina aminiwa katika kutunza siri ya kitubio.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.