2016-03-03 08:25:00

Watoto kiini cha Sala ya Kiekumene!


Maadhimisho ya Siku ya Sala ya Kiekumene inayoadhimishwa kila mwaka ifikapo Ijumaa ya kwanza ya mwezi Machi ambayo kwa mwaka huu inaongozwa na kauli mbiu “Anayempokea mmoja wapo ya watoto hawa, ananipokea mimi” ni mwaliko wa kufungua malango ya mioyo ili kujenga udugu, ushirikiano na kuoneshana mshikamano kwa kuanzia na maskini pamoja na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Kwa mara ya kwanza maadhimisho haya yalifanyika kunako mwaka 1927. Nchi mbali mbali zinashiriki katika Siku ya Sala ya Kiekumene.

Maadhimisho haya mwaka huu yanakwenda sanjari na maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu ambamo waamini kwa namna ya pekee wanaalikwa kuwa na mpango mkakati wa “Saa 24 kwa ajili ya Bwana” unaoadhimishwa kati ya tarehe 4 – 5 Machi 2016. Siku hii ya sala imeandaliwa na waamini kutoka Cuba ambao wanapembua kwa kina na mapana mateso, mahangaiko na fursa ambazo wanawake nchini Cuba wanakumbana nazo.

Katika maadhimisho haya kutakuwepo na mchango wa mshikamano na fedha fedha itakayopatikana itasaidia watu wenye shida. Hapa waamini wanahamasishwa kutumia vyema karama na vipaji vyao ili kukuza na kudumisha moyo na ari ya kiekumene inayowavuta na kuwaunganisha wengi sanjari na kuwa na makini katika kudumisha majadiliano ya kidini, ili kujenga umoja katika utofauti; utajiri mkubwa katika mchakato wa ujenzi wa umoja wa kitaifa na kimataifa.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.