2016-03-03 08:38:00

Mpango mkakati wa Saa 24 kwa ajili ya Bwana!


Baba Mtakatifu Francisko, Ijumaa tarehe 4 Machi 2016, kuanzia saa 11: 00 jioni kwa saa za Ulaya anatarajiwa kuongoza Ibada Upatanisho wa ujumla, itakayofuatiwa na maungamo na maondoleo ya dhambi ya mtu mmoja mmoja kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Ibada hii ni sehemu ya utekelezaji wa maagizo yaliyotolewa kwenye  Waraka wa Baba Mtakatifu Francisko Uso wa huruma “Misericordiae vultus” kwa ajili ya maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu.

Mpango mkakati wa “Saa 24 kwa ajili ya Bwana” unaadhimishwa Ijumaa na Jumamosi zinazotangulia Jumapili ya Nne ya Kipindi cha Kwaresima. Kila Jimbo linapaswa kufanya maadhimisho haya ili kuwapatia waamini nafasi ya kuweza kuchunguza dhamiri zao, kujuta, kuungama na hatimaye kutimiza malipilizi, ili kuambata huruma ya Mungu katika maisha yao. Sakramenti ya Upatanisho inagusa undani wa mtu kwani ni chimbuko la amani na utulivu wa ndani.

Mapadre waungamishaji  wanapaswa kuwa ni ishara halisi ya huruma na upendo wa Mungu unaosamehe na kuokoa. Mapadre wawe kweli ni watumishi waaminifu wa msamaha wa Mungu kwa kuwakumbatia wote: wema na wadhambi. Waamini wanapaswa kutambua kwamba leo hii hisia ya dhambi imepotea katika ulimwengu mamboleo, kiasi cha kuwafanya watu kusindwa kuona ukweli.

Kuna dhambi ya mauti inayomtenga mwamini na Mungu pamoja na Kanisa. Hii ni dhambi inayotendwa kwa uhuru kamili. Dhambi ndogo inajeruhi urafiki kati ya mwamini na Mwenyezi Mungu. Wataalam wa maisha ya kiroho wanasema kwamba, maungamo y amara kwa mara yanasaidia kujenga na kudumisha mahusiano mema na Kristo Yesu, tayari kuendeleza mchakato wa kuifia dhambi kila siku, ili kuishi ndani ya Kristo. Waamini waoneshe kusikitishwa kila wanapotenda dhambi, ili kuwa tayari kukimbilia na kuambata upendo wenye huruma ya Mungu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.