2016-03-02 12:16:00

Mchakato wa kukuza maendeleo na mapambano dhidi ya utumwa mamboleo


Askofu mkuu Paul Richard Gallagher, Katibu mkuu wa mambo ya nchi za nje na ushirikiano wa kimataifa mjini Vatican kuanzia tarehe 1- 3 Machi 2016 anafanya ziara ya kikazi nchini Uingereza kwa kukutana na kuzungumza na viongozi wakuu wa Serikali ya Uingereza na Jumuiya ya Madola pamoja na viongozi wa Makanisa nchini Uingereza ili kukusanya nguvu za pamoja katika mchakato wa ustawi na maendeleo ya wengi sanjari na kupambana kufa na kupona na biashara haramu ya binadamu inayoendelea kudhalilisha utu na heshima ya binadamu!

Askofu mkuu Gallagher anakaza kusema, mazungumzo na viongozi wakuu wa Serikali na Kanisa ni muhimu sana ili kwa pamoja kujenga mshikamano wa dhati utakaosaidia kupambana na umaskini kwa kuharakisha mchakato wa maendeleo ya mtu mzima: kiroho na kimwili. Haya ni mambo ambayo yanapswa kufanyiwa kazi na wala yasibaki tu kama nadharia. Serikali ya Uingereza ina mahusiano ya kidiplomasia na nchi mbali mbali duniani, kumbe, kwa kushirikiana diplomasia ya Vatican mchakato wa maendeleo unaweza kusonga mbele sanjari na kukomesha biashara haramu ya binadamu na viungo vyake.

Serikali ya Uingereza inaendelea kushirikiana na Vatican katika mapambano dhidi ya uhalifu wa utu na heshima ya binadamu kama anavyosema Baba Mtakatifu Francisko. Utumwa mamboleo ni kati ya matatizo na changamoto kubwa kwa Jumuiya ya Kimataifa. Chimbuko lake ni umaskini, vita, majanga asilia pamoja na mipasuko ya kijamii. Wagenge ya uhalifu wa kimataifa yanatumia mianya yote hii kupandikiza utamaduni wa kifo.

Kanisa Katoliki lina mtandao mkubwa wa huduma za maendeleo ya kijamii, kazi inayotekelezwa kwa namna ya pekee na mashirika ya huduma ya Kanisa Katoliki. Mashirika haya yakiwezeshwa kwa hali na mali, yanaweza kuwa msaada mkubwa katika mapambano ya umaskini duniani kwa kukuza na kudumisha utu, heshima, ustawi na maendeleo ya wengi.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.