2016-03-02 11:03:00

Mahakama ya huruma ya Mungu!


Kardinali Mauro Piacenza Mhudumu mkuu wa Toba ya Kitume, tarehe 29 Februari amefungua kozi maalum kwa ajili ya wahudumu wa Sakramenti ya Upatanisho, wakati huu Mama Kanisa anapowaalika watoto wake kujipatanisha na Mungu pamoja na jirani zao kwa njia ya toba na wongofu wa ndani. Kozi hii kwa sasa imeingia awamu ya 27 tangu ilipoanzishwa kama sehemu ya mchakato wa majiundo endelevu kwa Mapadre katika kutekeleza dhamana, wajibu na utume wao katika huduma ya Neno, Sakramenti za Kanisa na shughuli za kichungaji.

Kozi hii itahitimishwa hapo tarehe 4 Machi 2016 kwa kukutana na Baba Mtakatifu Francisko na jioni yake kushiriki katika Ibada ya toba ya jumla, kama sehemu ya maandalizi ya maadhimisho ya Fumbo la Pasaka, kilele cha huruma ya Mungu katika maisha ya mwanadamu! Katika maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu, kwa mwaka huu, kozi inajikita zaidi katika Sakramenti ya Upatanisho, mkazo unawekwa katika haki na wajibu wa muungamaji; mahusiano kati ya huruma ya Mungu, ukweli na haki; pamoja na majiundo makini ya dhamiri ya mwamini.

Kozi hii inachambua pia nafasi ya Padre muungamishaji kama shuhuda wa upendo na huruma ya Mungu; maongozi ya maisha ya kiroho; changamoto za kiutu na kimaadili katika ajenda ya usawa wa kijinsia. Haya ni mambo msingi yanayoweza kumsaidia Padre muungamishaji na mwamini anayetaka kukimbilia huruma ya Mungu kwa njia ya Sakramenti ya Upatanisho. Maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu ni fursa muafaka ya kutafakari kuhusu Fumbo la huruma ya Mungu liloshuhudiwa kwa namna ya pekee kwa njia ya mateso, kifo na ufufuko wa Kristo anayeishi na kulitegemeza Kanisa kwa njia ya Neno na Sakramenti zake.

Kardinali Mauro Piacenza anafafanua kwamba, Baba Mtakatifu Francisko kwa namna ya pekee kabisa anawaalika waamini katika maadhimisho ya Kwaresima ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu kutubu na kumwongokea Mungu ili kuona na kuonja Sura ya huruma ya Baba wa milele anayefuta uovu na kusamehe dhambi; asiyetunza hasira na anayependa kuhurumia na kusahau! Hapa kuna haja ya kujenga na kudumisha mshikamano na Khalifa wa Mtakatifu Petro ili kweli kipindi hiki cha Mwaka Mtakatifu kiweze kuwa ni chemchemi ya huruma na upendo wa Mungu kwa waja wake.

Sakramenti ya Upatanisho inapewa kipaumbele cha kwanza katika maisha na utume wa Kanisa anasema Kardinali Mauro Piacenza, lakini Wakleri wanayo dhamana kubwa zaidi katika utekelezaji wa dhamana hii kwani wao kweli ni mashuhuda na vyombo vya huruma ya Mungu. Wawe wa kwanza kumkimbilia Mwana Kondoo wa Mungu aondoaye dhambi za dunia; kwa toba na wongofu wa ndani. Huu ni mwaliko ambao Mama Kanisa anaendelea kuutoa kwa familia ya Mungu ili kuona na kutambua kwamba, Mwana Kondoo wa Mungu amateswa, akafa na kufufuka ili kumkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti.

Waamini watambue kwamba, kuna dhambi wanazotenda kwa mawazo, maneno, matendo na kutotimiza wajibu! Mambo yote haya yanawachangamotisha kukimbilia na kuambata huruma ya Mungu. Shetani anaendelea kuonesha makucha yake katika dhamiri za watu, kwa kuvuruga akili na utashi wao, kiasi kwamba, kanuni maadili na utu wema, vinakuwa havina nafasi tena katika mchakato wa kufikri na kutenda. Huu ndio mwanzo wa dhambi ya kutotii ambayo imekuwa ni chanzo cha mateso na mahangaiko ya binadamu. Kumbe, waamini wamkimbilie Mwana Kondoo wa Mungu aanayeondoa dhambi za dunia, watambue kwamba, kuna shetani na dhambi duniani.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.