2016-03-01 10:02:00

Zingatieni: utume, wongofu na umoja katika mawasiliano!


Padre Federico Lombardi baada ya kuitumikia Radio Vatican kama mkurugenzi wa vipindi na hatimaye kama Mkurugenzi mkuu, tarehe 29 Februari 2016 ameng’atuka rasmi kutoka madarakani pamoja na Dr. Alberto Gasbarri, Mkurugenzi wa utawala Radio Vatican. Tukio hili limeadhimishwa kwa Ibada ya Misa Takatifu iliyoongozwa na Padre Federico Lombardi na kuhudhuriwa na viongozi wakuu wa Sekretarieti ya Mawasiliano ya Vatican, wafanyakazi na wadau mbali mbali katika tasnia ya habari.

Katika mahubiri yake, Padre Lombardi amekazia kwa namna ya pekee mambo makuu matatu yanayopaswa kuvaliwa njuga na wafanyakazi wa Radio Vatican kwa sasa na kwa siku za usoni: utume wongofu na umoja, huku wakiwa na matumaini makubwa katika mchakato wa mabadiliko yanayoendelea kutekelezwa na Baba Mtakatifu Francisko katika maisha na utume wa Kanisa.

Padre Lombardi amewataka wafanyakazi wa Radio Vatican kutambua kwamba, wao wanatekeleza dhamana na utume wa kutangaza Habari Njema ya Wokovu kwa niaba ya Kanisa kwa kutumia Radio pamoja na maendeleo ya sayansi na teknolojia ili kuweza kuwafikia watu wengi zaidi, kadiri ya lugha na mahali walipo, daima lengo ni kugusa mambo msingi katika maisha ya binadamu kama alivyofanya Kristo mwenyewe.

Wafanyakazi wa vyombo vya mawasiliano ya jamii vinavyomilikiwa na kuendeshwa na Kanisa kwa njia ya wito, maisha na huduma yao, wanashiriki kikamilifu katika kazi ya ukombozi iliyoanzishwa na Kristo Yesu na kwa sasa inaendelezwa na Khalifa wa Mtakatifu Petro. Kumbe, wafanyakazi wa Radio Vatican wanashiriki kikamilifu katika utume huu!

Padre Lombardi anakaza kusema, kuna haja ya kuendelea kujikita katika mchakato wa toba na wongofu wa ndani kwa kuondokana na wasi wasi na woga usiokuwa na mashiko kutokana na mchakato wa mageuzi yanayoendelea kutekelezwa na Baba Mtakatifu Francisko katika maisha na utume wa Kanisa. Wafanyakazi wanahimizwa na Kristo kupyaisha maisha yao, kwa kuwajibika, kwa kuwa na imani na matumaini pasi na kukata wala kujikatia tamaa. Kipindi cha Kwaresima na kwa namna ya pekee, maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu iwe ni nafasi ya kusali na kutekeleza dhamana na utume huu kwa ari na moyo mkuu!

Padre Lombardi Lombardi ambaye kwa miaka 25 Radio Vatican imekuwa ni Jumuiya yake, amewataka wafanyakazi wa Radio Vatican kujenga na kuimarisha Jumuiya ya wanahabari, tayari kutoka kifua mbele, ili kushiriki katika utangazaji na ushuhuda wa Habari Njema miongoni mwa watu wa mataifa kama anavyokaza kusema Baba Mtakatifu Francisko. Hii ni Jumuiya ambayo kwa sasa inakabiliwa na mageuzi makubwa katika maisha na mfumo wake. Jumuiya hii ioneshe na kushuhudia umoja na Baba Mtakatifu chini ya usimamizi wa Sekretarieti ya mawasiliano, kwa kuwa na imani na matumaini. Padre Lombardi anawaombea: hekima, neema na busara waliokabidhiwa dhamana hii nyeti na Baba Mtakatifu Francisko kutekeleza wajibu wao barabara. Amewashukuru wote waliomwezesha kutekeleza dhamana na utume wake kwenye Radio Vatican kwa kipindi chote hiki cha miaka 25.

Mara baada ya maadhimisho ya Ibada ya Misa takatifu, wafanyakazi wa Radio Vatican pamoja na waalikwa waliingia katika awamu ya pili ya shukrani kwa Padre Lombardi na Dr. Alberto Gasbarri ambaye amekaza kusema, mawasiliano ni kiini, maisha na utume wa Kanisa. Amewashukuru  Wayesuit ambao kwa kipindi cha takribani miaka 50 wamejisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya utume, ustawi na maendeleo ya Radio Vatican. Kanisa linatumwa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu. Ni matumaini ya Dr. Gasbarri kwamba, Monsinyo Dario Viganò ataweza kufanya maboresho makubwa pale ambapo uongozi unaong’atuka kutoka madarakani pengine ulishindwa kutekeleza.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.