2016-03-01 09:24:00

Askofu ni mwalimu na chombo cha huruma ya Mungu!


Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican, tarehe 27 Februari 2016 amemweka wakfu Monsinyo Paul Tighe, kuwa Askofu, tukio ambalo limehudhuriwa na ujumbe mzito kutoka Ireland. Itakumbukwa kwamba, hivi karibuni, Baba Mtakatifu Francisko alimteua Askofu Paul Tighe kuwa Katibu mwambata wa Baraza la Kipapa la Utamaduni baada ya kutumikia Baraza la Kipapa la Mawasiliano ya Jamii kama Katibu mkuu.

Daraja la Uaskofu ni zawadi ambayo Mwenyezi Mungu anaitoa kwa Kanisa lake, ili kuendeleza utume wa kufundisha, kuongoza na kuwatakatifuza Watu wa Mungu; kazi waliochiwa Mitume, dhamana inayoendelezwa na waandamizi wao. Askofu anawekwa wakfu ili kumshuhudia Kristo mfufuka sanjari na kuendeleza umoja na utume wa Kanisa. Askofu anatakiwa kuongoza kwa kutumia busara inayobubujika kutoka katika Injili ya Kristo kwa kuonesha pia ushirikiano wa karibu na Khalifa wa Mtakatifu Petro katika uongozi wa Kanisa la Kiulimwengu.

Askofu anahamasishwa kuwa ni mwalimu wa kweli, kwa kuonesha na kufundisha uvumilivu na mafundisho tanzu ya Kanisa pamoja na sababu ya matumaini yaliyomo mioyoni mwao, daima akiwa shuhuda na chombo cha huruma ya Mungu; maisha yanayoangaziwa na mwanga wa Injili ya Kristo na kumwilishwa katika umoja na udugu.

Askofu anapaswa kuonesha upendo wa hali ya juu kwa Kristo na  Kanisa lake; kwa kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya maskini na wale wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii, huku akiendelea kuboresha upendo huu kwa njia ya Sakramenti za Kanisa, Tafakari ya Neno la Mungu na Maisha ya Sala yanayojikita katika imani na huruma ya Mungu. Kauli mbiu ya Askofu Paul Tighe ni”Estote factores Verbi”  yaani “Iweni watu wa matendo”. Hii ni changamoto ya kuendeleza mchakato wa majadiliano katika ngazi mbali mbali; majadiliano na tamaduni za watu, ili kukoleza mchakato wa utamadunisho, ili kweli Neno la Mungu liweze kukita mizizi yake katika maisha na tamaduni za watu mintarafu ufunuo wa Kristo ambaye ni kielelezo makini cha huruma, uaminifu na sadaka ya Baba wa milele.

Kardinali Parolin anawataka waamini kuwa na imani thabiti kwa Kristo na Kanisa lake, kwa kuzaa matunda ya toba na wongofu wa ndani. Pale wanapojisikia wametindikiwa na neema na baraka kutoka kwa Kristo, basi wawe wepesi kukimbilia katika kiti cha huruma ya Mungu, ili Kristo mwenyewe aweze kuwaganga na kuwaponya. Maaskofu wawasaidie waamini wao kupata mbolea bora ya Neno la Mungu, Sakramenti za Kanisa, huruma na upendo, ili waweze kuzaa matunda mengi na yenye ubora. Askofu aoneshe sura na sifa ya Baba mwema. Askofu anahimizwa kuhubiri na kulishuhudia Neno la Mungu katika maisha yake, ili watu waonje uwepo wa Kristo anayejisadaka na kuwashirikisha Injili ya furaha, msamaha na amani ya ndani.

Kardinali Parolin anampongeza Askofu Tighe ambaye katika kipindi cha miaka 33 ya Upadre wake amefundisha katika vyuo vikuu mbali mbali nchini Ireland; amekuwa mkurugenzi wa Idara ya mawasiliano Jimbo kuu la Dublin na kunako mwaka 2007 Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto XVI akamteuwa kuwa Katibu mkuu wa Baraza la Kipapa la Mawasiliano ya Jamii na Mwaka 2014 Papa Francisko akamteuwa kuwa Katibu mkuu wa Tume ya Mawasiliano mjini Vatican. Utume huu unaonesha mahusiano kati ya imani, siasa na tamaduni katika nyanja ya mawasiliano. Kwa kuwekwa wakfu kama Askofu anaanza ukurasa mpya wa maisha na utume wake.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.