2016-02-29 07:23:00

Tubuni na kumwongokea Mungu!


Maafa na majanga mbali mbali ni kati ya habari ambazo zinaendelea kutanda katika vyombo vya habari kama ilivyokuwa kwenye Agano Jipya kuhusiana na watu waliongukiwa na mnara wa Sloam au wale watu kumi na wa nane waliokuwa wameuwawa kikatili, matukio ambayo Mwinjili Luka anayaweka mbele ya macho ya wasomaji wake, Jumapili ya tatu ya Kipindi cha Kwaresima kwa kutaka kumweka Yesu katika majaribu. Yesu alitambua nia na tafsiri yao mbaya kwamba, matukio haya yalikuwa ni kuonesha hasira ya Mungu kutokana na dhambi walizokuwa wametenda na wale waliosalimika kujiona kuwa walikuwa wanastahili.

Yesu anapinga mwelekeo huu wa Mungu kutoa adhabu ya maafa kwa wale wanaotenda dhambi na kuwaalika wote kutambua kwamba, wanahitaji kutubu na kumwongokea Mungu kwani watu wote ni wa dhambi mbele ya Mungu. Watu wasipotubu na kumwongokea Mungu watakufa kama inavyosimuliwa na Mwinjili Luka. Huu ndio mwelekeo hata leo hii wa binadamu kutaka kukimbia wajibu kwa kumshirikisha mungu waliye muumba kwa mfano na sura yao ya kibinadamu.

Yesu anawaalika waamini kuwa na mwelekeo mpya katika maisha yao ya kiroho kwa kuachana na dhambi ili hatimaye, kuambata Injili ya Kristo, mchakato unaojikita katika toba na wongofu wa ndani. Hii ni sehemu ya tafakari iliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, Jumapili tarehe 28 Februari 2016. Ni changamoto na mwaliko wa kuzaa matunda hasa wakati huu wa maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu.

Hiki ni kipindi cha neema; kipindi cha Fumbo la Kristo na Kanisa kabla Kristo Yesu hajarudi tena kuwahukumu wazima na wafu. Ni wakati muafaka wa kuonja huruma na uvumilivu wa Mungu kwa wa dhambi na kwamba, hakuna mtu ambaye amechelewa hata kidogo kutubu na kumwongokea Mungu ambaye ni mvumilivu na mpole, daima anamsubiri mdhambi hata katika dakika ya mwisho ya maisha yake. Mungu anamwokoa mdhambi kwani ana upendo wa dhati kwa waja wake, kielelezo cha huruma yake isiyokuwa na mipaka.

Lakini, Baba Mtakatifu Francisko anakaza kusema, kuna haja ya kufanya haraka kutubu na kumwongokea Mungu. Waamini wakimbilie tunza na ulinzi wa Bikira Maria, ili aweze kuwaombea kwa Mwenyezi Mungu ili awafungulie malango ya mioyo yao, tayari kupokea neema na huruma ya Mungu bila kuwahukumu wengine, bali kuchunguza dhamiri ili kutubu na kumwongokea Mungu katika maisha.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.