2016-02-29 16:06:00

Kimbilieni huruma ya Mungu!


Kwaresima ni kipindi cha siku arobaini kinachowasaidia Wakristo kujiandaa kikamilifu kwa ajili ya maadhimisho ya Fumbo la Pasaka, yaani, mateso, kifo na ufufuko wa Kristo. Kwaresima ya mwaka 2016 inachukua uzito wa pekee kwani inakwenda sanjari na maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu. Hiki ni kipindi cha toba na wongofu wa ndani, mwaliko na changamoto kwa Wakristo kukimbilia huruma na upendo wa Mungu katika maisha yao.

Ni kipindi cha kutafakari na kumwilisha Neno la Mungu katika uhalisia wa maisha, kielelezo cha imani tendaji. Kwaresima ni kipindi cha sala inayoshuhudiwa katika matendo ya huruma kiroho na kimwili. Ni kipindi cha kufunga na kujinyima kama sehemu ya mchakato wa kuratibu vilema vya maisha ya binadamu kwa kuonesha pia jicho la huruma kwa jirani! Kwaresima ni muda muafaka wa kujenga na kuimarisha mshikamano ndani ya familia kwa kuambata pia maisha ya sala na Sakramenti za Kanisa.

Hizi ni changamoto zinazotolewa na Askofu Michael Msonganzila wa Jimbo Katoliki Musoma, Tanzania wakati huu wa kipindi cha Kwaresima, sanjari na maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu. Baba Mtakatifu Francisko kwa namna ya pekee, anawaalika waamini kujikita katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili kama njia mahususi ya kuadhimisha Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu.

Waamini wajenge ari na moyo wa kupendana, kuhurumiana na kusameheana, ili kuonja huruma ya Mungu katika maisha yao. Waamini wawe na ujasiri wa kuona na hatimaye kukiri mapungufu yao kwa kukimbilia kiti cha huruma ya Mungu ambacho ni Sakramenti ya Upatanisho inayowaonjesha huruma na upendo wa Mungu usiokuwa na mipaka. Waamini wakishaonjeshwa huruma ya Mungu, wawe wapesi kuwahurumia na kuwasamehe jirani zao.

Askofu Msonganzila anawaalika waamini kipindi hiki cha Kwaresima kuzama zaidi katika maisha ya sala na tafakari, ili kujenga mahusiano ya ndani zaidi na Mwenyezi Mungu. Kuacha dhambi na ubaya wa moyo kuna gharama na kwamba, haya ni mapambano endelevu yanayomtaka mwamini kujikita katika sala, toba na wongofu wa ndani. Vinginevyo anasema Askofu Msonganzila, waamini watajikuta wakiwa ni watumwa wa shetani na mambo yake. Kwaresima ni kipindi cha kufunga na kujinyima kwa ajili ya kuwasaidia maskini na wale wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii!

Na Veronica Modest,

Musoma.








All the contents on this site are copyrighted ©.