2016-02-29 07:42:00

Kanisa katika huduma ya upendo kwa wakimbizi na wahamiaji!


Kardinali Luis Antonio Tagle, Rais wa Shirikisho la Mashirika ya Misaada ya Kanisa Katoliki Kimataifa, Caritas Internationalis, kuanzia tarehe 28 hadi tarehe 2 Machi 2016 anatembelea Lebanon ili kushuhudia jinsi ambavyo Mashirika ya Misaada ya Kanisa Katoliki huko Mashariki ya Kati yanavyojitahidi kuwasaidia wakimbizi na wahamiaji kutoka Syria, na Iraq wanaohudumiwa huko Yordani Lebanon na Uturuki. Takwimu zinaonesha kwamba, hadi sasa kuna zaidi ya wakimbizi na wahamiaji millioni 5 wanaohudumiwa na Mashirika ya Misaada.

Lebanon peke yake inatoa hifadhi kwa wakimbizi na wahamiaji millioni moja kati ya wananchi millioni nne kutoka Lebanon. Changamoto ya wakimbizi inaonekana kuwa ni kubwa kwa Jumuiya ya Ulaya kiasi kwamba, nchi nyingi zimeanza kufunga mipaka yake baada ya wakimbizi na wahamiaji millioni moja kuwasili Barani Ulaya, ili kutafuta hifadhi na usalama wa maisha yao. Mashirika ya Misaada ya Kanisa Katoliki yanaendelea kutoa chakula, malazi, dawa pamoja na huduma za kisheria na ushauri nasaha.

Caritas Internationalis inaendelea kukazia umuhimu wa watoto na vijana kupewa fursa ya kujiendeleza katika elimu, ili kuwajengea matumaini ya leo na kesho iliyo bora zaidi kwa njia ya elimu makini. Kuna hofu kwamba, watoto wengi nchini Syria watakosa nafasi ya masomo hali ambayo inaweza kuchangia ugumu wa maisha kwa siku za usoni. Caritas Lebanon inatoa msaada pia kwa wakimbizi na wahamiaji kutoka Iraq. Caritas Internationalis imepewa dhamana ya kuratibu misaada ya Mashirika ya Kanisa Katoliki katika huduma kwa wakimbizi na wahamiaji huko Mashariki ya Kati. Caritas pia inaendesha kampeni ya kusitishwa kwa vita huko Syria, ili haki, amani na upatanisho wa kitaifa, viweze kuanza kushika mkondo wake katika akili na nyoyo za watu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.