2016-02-29 07:32:00

Changamoto ya huduma kwa wakimbizi na wahamiaji Barani Ulaya


Baba Mtakatifu Francisko mara baada ya Sala ya Malaika wa Bwana, Jumapili tarehe 28 Februari 2016 kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican aliyaelekeza macho yake kwenye mateso na mahangaiko ya wakimbizi na wahamiaji, lakini kwa namna ya pekee kabisa wakimbizi na wahamiaji waliokwama huko Ugiriki na nchi nyingine jirani ambazo zimekuwa mstari wa mbele katika kuwapokea na kuwahudumia wakimbizi na wahamiaji kwa moyo wa ukarimu.

Baba Mtakatifu kwa namna ya pekee anapenda kuialika Jumuiya ya Kimataifa kuonesha ushirikiano na mshikamano katika kuwahudumia wakimbizi na wahamiaji; kwa kuwa na mgawanyo bora zaidi kati ya nchi mbali mbali sanjari na kuendeleza majadiliano.

Baba Mtakatifu ameonesha pia matumaini yake kutokana na tamko la kusitisha mashambulizi huko Syria na kwamba, anapenda kutumia fursa hii kuwaalika wadau mbali mbali kuheshimu makubaliano haya, ili hatimaye, wananchi wa Syria waweze kupata nafuu na huo uwe ni mwanzo wa majadiliano ya kufikia muafaka wa amani, jambo linalotamaniwa na wananchi wengi wa Syria.

Baba Mtakatifu ametumia nafasi hii pia kuonesha ukaribu wake kwa wananchi wa Kisiwa cha Fiji waliokumbwa na tufani kubwa ambayo imesababisha maafa kwa watu na mali zao. Anapenda kuwaimarisha wale wote wanaoendelea kutoa huduma kwa waathirika. Mwishoni, Baba Mtakatifu ametambua uwepo wa wenyeji kutoka Biafra, Nigeria wanaoishi kwa sasa ughaibuni.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.