2016-02-27 08:11:00

Rushwa na ufisadi ni hatari kwa demokrasia!


Baraza la Maaskofu Katoliki Benin linasema rushwa na ufisadi ni sumu kubwa dhidi ya haki na demokrasia nchini humo, changamoto kwa Familia ya Mungu nchini Benin kusimama kidete kupinga tabia ya kutoa na kupokea rushwa hasa wakati huu Benin inapojiandaa kufanya uchaguzi mkuu hapo tarehe 28 Februari 2016. Rais Thomas Yayi Boni anatarajiwa kumaliza muda wake wa uongozi na kadiri ya Katiba ya nchi hatakuwa na sifa tena ya kuchaguliwa kuongoza nchi baada ya kuongoza katika vipindi viwili kwa muda wa miaka kumi.

Baraza la Maaskofu Katoliki Benin linakaza kusema, saratani ya rushwa na ufisadi imekuwa ni kikwazo kikuu cha maendeleo na ustawi wengi, kiasi kwamba, Kanisa linalazimika kuingilia kati, ili kukuza na kudumisha kanuni maadili, haki na amani, kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya wananchi wengi. Maaskofu Katoliki Benin wameyasema haya katika mjadala wa hadhara uliowashirikisha wadau mbali mbali waliofikia uamuzi wa kumwandikia barua ya wazi, Rais Thomas Yayi Boni, ili kulivalia njuga tatizo la rushwa.

Ili kufanikisha mchakato mzima wa upigaji kura nchini Benin, Baraza la Maaskofu Katoliki Benini linawataka wadau wote kuhakikisha kwamba, wanawashirikisha wananchi kupambana na rushwa ambayo kwa sasa inachangia kuporomoka kwa demokrasia, haki na amani nchini Benin. Uchu wa mali na madaraka ni mambo yanayofumbatwa katika ubinafsi kiasi hata cha kuathiri ustawi wa nchi. Baraza la Maaskofu Katoliki Benin linawaalika waamini wakati huu wa maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu kutubu na kumwongokea Mungu, kwa kujikita katika msamaha na upatanisho wa kweli.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.