2016-02-27 14:29:00

Rais Mauricio Macri wa Argentina akutana na Papa Francisko


Baba Mtakatifu Francisko, Jumamosi tarehe 27 Februari 2016 amekutana na kuzungumza na Rais Mauricio Macri wa Argentina aliyechaguliwa hivi karibuni, ambaye baadaye amekutana na kuzungumza pia na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican aliyekuwa ameambatana na Askofu mkuu Paul Richard Gallagher, Katibu mkuu wa Mambo ya nchi za nje na ushirikiano wa kimataifa mjini Vatican.

Baba Mtakatifu pamoja na mgeni wake wameridhishwa na mahusiano mazuri yaliyopo kati ya nchi hizi mbili na baadaye wamejadili kwa kina na mapana masuala mbali mbali yenye mafao kwa pande hizi mbili katika mchakato wa maendeleo ya mtu mzima: kiroho na kimwili; haki msingi za binadamu; mapambano dhidi ya umaskini, biashara na matumizi haramu ya dawa za kulevya; haki, amani na upatanisho wa kijamii. Viongozi hawa wawili wameridhishwa na mchango wa Kanisa nchini Argentina katika utoaji wa huduma msingi na majiundo makini kwa vijana wa kizazi kipya; huduma inayotolewa na taasisi za elimu zinazomilikiwa na kuendeshwa na Kanisa Katoliki nchini Argentina, bila kusahau mchango wa Kanisa katika shughuli za uzalishaji. Mwishoni, viongozi hawa wamejadili pia masuala yenye mafao ya kikanda na kimataifa.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.