2016-02-27 09:20:00

Njia ya Msalaba na huruma ya Mungu!


Baba Mtakatifu Francisko amemteua Kardinali Gualtiero Bassetti, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Perugia, Italia kuandaa tafakari ya Njia ya Msalaba kuzunguka Magofu ya Colosseo mjini Roma, Ijumaa kuu, hapo tarehe 25 Machi 2016. Hii njia ya Msalaba inayozingatia Vituo 14 kadiri ya Mapokeo ya Kanisa. Kwa namna ya pekee, mwaka huu, Njia ya Msalaba inapania kugusa mateso na mahangaiko ya binadamu katika ulimwengu mamboleo.

Matatizo na changamoto za maisha ya kifamilia; dhuluma na nyanyaso, ili wote hawa waweze kuonja upendo na huruma ya Mungu, hususan wakati huu Mama Kanisa anapoadhimisha Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu. Kardinali Bassetti anasema kwamba, tafakari ya Njia ya Msalaba inajikita katika Neno la Mungu linalomwilishwa katika uhalisia wa maisha ya watu. Vita, umaskini, magonjwa, dhuluma, nyanyaso, mauaji ni kati ya mambo ambayo yanaendelea kudhalilisha utu na heshima ya binadamu.

Fumbo la Msalaba, yaani mateso kifo na ufufuko wa Kristo, ni chemchemi ya matumaini kwa watu wanaoteseka sehemu mbali mbali za dunia. Njia ya Msalaba inapania pamoja na mambo mengine kuunganisha mateso ya familia ya binadamu na yale ya Kristo pale Msalabani. Ulimwengu mamboleo umesheheni Misalaba ambayo watu wa Mungu wanaibeba kila siku ya maisha yao, mwaliko wa kuangalia mateso na changamoto za maisha katika mwanga wa huruma na mapendo ya Mungu, ili kweli mateso haya yaweze kupata maana kamili katika maisha ya watu; yaani ni mateso yanayoleta ukombozi.

Maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu ni kipindi muafaka cha kutafakari huruma na upendo wa Mungu kwa binadamu! Matatizo na changamoto za maisha ya kifamilia, zimepewa uzito wa pekee katika kituo cha Nne cha Njia ya Msalaba, pale Yesu anapokutana na Mama yake Bikira Maria. Hapa familia nyingi zinapata utambulisho wake; ukosefu wa fursa za ajira kwa vijana; utakaso na upatanisho ndani ya Kanisa ni mambo ambayo pia yamezingatiwa katika tafakari ya Njia ya Msalaba.

Kardinali Bassetti anakaza kusema, Fumbo la Msalaba ni kielelezo cha utakaso na upatanisho kati ya binadamu na Muumba wake. Upatanisho ni changamoto kubwa kwa mtu binafsi, jamii, Kanisa na Familia ya binadamu katika ujumla wake, ili kuwajengea tena watu imani na matumaini katika Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo unaofumbatwa katika sera za utoaji mimba, matumizi haramu ya dawa za kulevya; vita na nyanyaso; maafa na majanga katika maisha ya watu. Wote hawa wanahamasishwa kuutafuta Uso wa huruma ya Mungu. Mauaji ya Wakristo sehemu mbali mbali za dunia ni kielelezo cha ushuhuda wa imani kwa Kristo na Kanisa lake, changamoto ya kujenga na kudumisha Uekumene wa damu. Maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu ni mwaliko wa kutafakari na kumwilisha changamoto mbali mbali katika maisha ya mwanadamu kwa njia ya mwanga wa huruma ya Mungu.

Kifo cha Yesu Kristo Msalabani ni kielelezo cha hali ya juu kabisa cha upendo na huruma ya Mungu; fumbo la imani, maisha na utume wa Kanisa. Kifo bado linaendelea kuwa ni fumbo linalotikisha msingi wa maisha na imani ya watu wengi hususan katika familia, kiasi cha kuwaacha watu wengi wakiwa na maswali yasiyokuwa na majibu! Lakini kwa Mkristo jibu linapatikana pale Msalabani, Kristo Yesu alipoinamisha kichwa na kutoa roho yake! Mateso, kifo na ufufuko wa Kristo ni chemchemi ya ukombozi wa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti. Njia ya Msalaba kwa Mwaka wa huruma ya Mungu ni tafakari ya mateso, mahangaiko na matumaini ya binadamu yanayofumbata huruma na upendo wa Mungu. Fumbo la Pasaka ni kielelezo cha hali ya juu kabisa cha huruma ya Mungu na matumaini kwa binadamu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.