2016-02-27 08:51:00

Dini ni mdau wa maendeleo endelevu!


Baraza la Makanisa Ulimwenguni, WCC hivi karibuni limeendesha mkutano wa kimataifa mjini Berlin, Ujerumani uliokuwa unaongozwa na kauli mbiu “Wadau wa mabadiliko: Dini na ajenda za maendeleo endelevu kwa Mwaka 2030”. Wajumbe wa mkutano huu wamekiri mchango mkubwa unaotolewa na dini katika kukuza na kudumisha mchakato wa maendeleo endelevu kwa binadamu kwa kuzingatia mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili. Dini ni chemchemi ya tunu msingi za maisha, maadili na utu wema. Wajumbe wanaihamasisha Jumuiya ya Kimataifa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa binadamu na mahitaji ya msingi katika sera na mikakati ya maendeleo endelevu.

Dr. Olav Fykse Tveit, Katibu mkuu wa Baraza la Makanisa Ulimwenguni akiratibu mkutano huu amesema kwamba, mwelekeo wa jumla wa masuala msingi yanayomgusa mwanadamu, kimsingi yanaratibiwa na imani. Lengo ni kuhakikisha kwamba, mikakati hii inawapatia watu matumaini ya maendeleo sanjari na kutumia rasilimali na utajiri uliopo kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya wengi.

Ajenda ya Maendeleo endelevu kwa Mwaka 2030 iliyopitishwa na Baraza kuu la Umoja wa Mataifa inatoa kipaumbele cha pekee kwa mambo msingi yanayopaswa kuvaliwa njuga na Jumuiya ya Kimataifa ili kuweza kuupatia umaskini kisogo; kupambana na ukosefu wa usawa sanjari na kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi ambayo kwa sasa kimekuwa ni kikwazo kingine cha maendeleo ya binadamu.

Wajumbe wa mkutano huu wamekiri na kupongeza mchango unaotolewa na dini mbali mbali katika kukabiliana na changamoto za maendeleo kwa binadamu: kiroho na kimwili. Katika nchi zinazoendelea dini na mashirika yake yamechangia kwa kiasi kikubwa katika sekta ya elimu, afya, maendeleo ya wanawake na watoto pamoja na kutoa huduma za kijamii kwa maskini, wagonjwa, wazee na walemavu. Kutokana na mchango huu, Jumuiya ya Kimataifa haina budi kushirikisha dini mbali mbali kama wadau wa maendeleo endelevu ya binadamu, katika kutafuta, kulinda na kudumisha haki, amani na maridhiano kati ya watu.

Dini hazina budi kuendelea kutoa mchango katika mapambano dhidi ya umaskini na kusaidia utekelezaji wa sera za maendeleo jamii. Dini kama wadau wa maendeleo endelevu anasema Dr. Tveit inaweza kuchangia kikamilifu, ikiwa kama kanuni maadili na tunu msingi za kidini zitapokelewa na wadau wengine wa maendeleo ya binadamu, bila kutumia ajenda za maendeleo kwa ajili ya kujiimarisha kisiasa badala ya kukazia maendeleo endelevu ya mtu mzima: kiroho na kimwili. Dini mbali mbali zimekuwa mstari wa mbele katika mapambano dhidi ya umaskini, ujinga na maradhi; zimesaidia mchakato wa utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote na bado zinaendelea kuhamasisha majadiliano ya kidini, ili amani, ustawi na maendeleo ya kweli viweze kupatikana.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.