2016-02-26 15:53:00

Upendo ni fadhila na utambulisho wa Kanisa!


Upendo na ukweli ni chanda na pete, chachu muhimu sana katika mchakato wa ujenzi wa dunia mpya inayojikita katika upendo kwa Mungu na jirani; mambo msingi yanayofumbatwa katika Fumbo la Utatu Mtakatifu. Hiki ni kiini cha Waraka wa kichungaji wa Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto XVI katika Mungu ni upendo, “Deus Caritas Est”  tema ambayo inachambuliwa na washiriki wa kongamano la kimataifa lililoandaliwa na Baraza la Kipapa linaloratibu misaada ya Kanisa Katoliki, Cor Unum, kuanzia tarehe 25 – 26 Februari 2016 kwa kuongozwa na kauli mbiu “Upendo haupungui neno wakati wowote”.

Kardinali Gerhard Muller, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la mafundisho tanzu ya Kanisa katika tafakari yake kwenye kongamano hili anasema, upendo kwa Mungu na jirani ni kiini cha huruma ya Mungu inayomwilishwa katika uhalisia wa maisha ya mwanadamu; jambo ambalo lilipewa kipaumbele cha kwanza na Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto XVI. Katika maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa huruma ya Mungu, Baba Mtakatifu Francisko anakazia kwa namna ya pekee huruma ya Mungu kama kielelezo na utambulisho wa maisha na utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro.

Kardinali Muller anaendelea kufafanua kwamba, upendo ni kiini cha maisha na utume wa Kanisa, changamoto kwa waamini kuhakikisha kwamba, upendo unakuwa ni sehemu ya vinasaba vya huduma inayotolewa na Mama Kanisa katika ulimwengu mamboleo kama ilivyo katika utangazaji wa Habari Njema kwa njia ya ushuhuda wa maisha na maadhimisho ya Sakramenti za Kanisa. Upendo ni fadhila ambayo inapaswa kuwa kweli ni utambulisho wa maisha na utume wa Kanisa kama taasisi na kama Jumuiya ya waamini.

Huu ndio mwelekeo wa kitaalimungu na kikanisa unaofumbatwa katika Waraka wa Mungu ni upendo, “Deus Caritas Est”. Hii pia ni chachu ya mageuzi yanayoendelea kutekelezwa na Baba Mtakatifu Francisko kwenye Sekretarieti kuu ya Vatican. Mungu ni upendo unaomwambata mwanadamu katika hija ya maisha yake hapa duniani. Upendo huu umeoneshwa kwa namna ya pekee kwa Neno wa Mungu kufanyika mwili na kukaa kati ya watu wake na kilele cha upendo huu, kinajionesha katika Fumbo la Msalaba, yaani mateso, kifo na ufufuko wa Kristo, kielelezo cha hali ya juu kabisa cha huruma ya Mungu kwa waja wake.

Kristo Yesu amefundisha na kushuhudia upendo kwa njia ya Fumbo la Msalaba na huduma kwa kuwaosha miguu mitume wake, ili nao pia waweze kuwa ni vyombo na mashuhuda wa huduma ya upendo kwa ndugu zao. Kumbe, mambo makuu matatu yanapaswa kuzingatiwa katika maisha na utume wa Kanisa yaani: Liturujia, Ushuhuda na huduma. Huduma ni kielelezo cha upendo wa Kristo na Kanisa; chachu ya kukua na kukomaa kwa Jumuiya ya Kikristo kama inavyojionesha katika Kitabu cha Matendo ya Mitume. Upendo unaonesha mambo msingi katika imani ya Kikristo kwa kutoa kipaumbele cha pekee kwa maskini na wale wanaosukumiwa pembezoni mwa jamii. Ushuhuda na huduma ya upendo ni kati ya mambo yaliyoliwezesha Kanisa la mwanzo kukua na kuongezeka kwa haraka, kiasi kwamba, Kanisa likawa kweli ni familia ya Mungu duniani. Wakristo wakaonja mateso ya jirani zao kiroho na kimwili na huko wakamwona na kumshuhudia Kristo Yesu. Mwanadamu amepitia mifumo mbali mbali ya maisha, kiasi kwamba, leo hii ubepari unaojikita katika faida kubwa unaendelea kutawala.

Hapa kuna haja ya kushuhudia na kumwilisha Mafundisho Jamii ya Kanisa yanayojikita katika: utu na heshima ya binadamu; mshikamano, haki na mafao ya wengi; kwani Kanisa ni Sakramenti ya wokovu kwa wote. Matendo ya huruma yanayopewa msukumo wa pekee na Baba Mtakatifu Francisko kwa wakati huu ni changamoto ya kutoa kipaumbele cha kwanza kwa binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu na kwamba, huduma ya upendo haina lengo la kuwaongoa watu kwa nguvu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.