2016-02-23 13:53:00

Watanzania wachangia millioni 86 kwa waathirika wa mafuriko Iringa


Waziri mkuu wa Tanzania Kasim Majaliwa amekutana na kufanya mazungumzo na mabalozi watatu kutoka nchi za Uturuki, Ireland na Uswisi pamoja na Mratibu Mkazi wa Umoja wa Mataifa hapa nchini.Akizungumza kwa nyakati tofauti na mabalozi Jumanne, Februari 23, 2016, ofisini kwake, Magogoni jijini Dar es Salaam, Waziri Mkuu aliwashukuru mabalozi hao kwa kuja kujitambulisha rasmi na kwa pongezi walizokuja kumpatia na kuahidi ushirikiano zaidi pamoja na nchi hizo.

Mapema leo, Waziri Mkuu alikutana na Mratibu Mkazi wa Umoja wa Mataifa hapa nchini, Bw. Alvaro Rodriguez ambaye alimweleza jinsi UNDP imekuwa ikisaidia programu za kukabiliana na maafa (resilience), ukuaji wa uchumi, utawala bora na masuala ya jinsia. Alisisitiza haja ya Tanzania kuendeleza kampeni ya kupambana na ujangili na kusisitiza kuwa Umoja huo una nia ya kusaidia utekelezaji wa Mpango wa Taifa wa Maendeleo wa Miaka Mitano.

Naye Balozi wa Uturuki, Bibi Yesemin Eralp alimweleza Waziri Mku nia ya nchi kuleta wawekezaji katika nyanja za kilimo, nishati, afya na ujenzi na kusisitiza kuwa kuna haja ya kufungua ubalozi wa Tanzania nchini kwao ili kuimarisha uhusiano uliopo. “Tunao uwezo wa kifedha na tunao uwezo wa kitaalamu na kiteknolojia. Tukifungua viwanda hapa nchini, tunaweza kuongeza ajira kwa Watanzania,” alisema.

Naye Balozi wa Ireland nchini, Bibi Fionnuala Gilsenan alimweleza Waziri Mkuu jinsi ambavyo nchi yake imekuwa ikisaidia sekta za kilimo kupitia mpango wa ASDP, bajeti ya Serikali na suala la lishe na urutubishaji wa vyakula (food nutrition and fortification). “Tulianza na suala la kilimo na bajeti ya Serikali. Hivi sasa tunataka kusaidia kwenye uelimishaji juu ya haki za wanawake, masuala ya uzazi wa mpango, pamoja na kupambana na ndoa za utotoni,” alisema.

“Tumeamua kupigia kelele suala la lishe na urutubishaji wa vyakula kwa sababu lishe duni imechangia kwa kiasi kikubwa udumavu wa watoto wengi. Tulipoanza tatizo hili lilikuwa limeenea kwa asilimia 46 kwa watoto walio chini ya umri wa miaka mitano lakini sasa limepungua na kufikia asilimia 36 hadi 38,” aliongeza. Alimuomba Waziri Mkuu Majaliwa alishikie bango suala hilo kwa Wakuu wa Mikoa na Wakuu wa Wilaya kote nchini kwani mtoto akishadumaa kimakuzi hata akili yake pia inadumaa na tatizo lake haliwezi kurekebishwa kwa tiba yoyote ile.

Naye Balozi wa Uswisi nchini, Bibi Florence Mattli alimweleza Waziri Mkuu nia ya nchi yake kudumisha ushirikiano na Tanzania ambao umedumu kwa miaka 50 ili kukuza viwango vya uchumi na kuleta maendeleo kwa Watanzania. Alimweleza Waziri Mkuu jinsi nchi yake imekuwa ikisaidia kundeleza nyanja za kupambana na rushwa kupitia TAKUKURU na kampeni ya kusaidia kujenga uelewa wa wananchi kupitia vyombo vya habari nchini.

Wakati huo huo, Waziri mkuu wa Tanzania Kassim Majaliwa amepokea misaada mbalimbali yenye thamani ya sh. milioni 85.88/- kwa ajili ya wananchi walioathirika na mafuriko kwenye vijiji vya kata ya Mlenge, tarafa ya Pawaga, wilaya ya Iringa vijijini mkoa wa Iringa. Misaada hiyo imetolewa na wadau mbalimbali kutokana na mafuriko ambayo yalibomoa   nyumba 82 katika kitongoji cha Kilala, kijiji cha Kisanga na kuwaacha wananchi wake bila makazi. Akizungumza na wananchi wa kijiji cha Kasanga ambako alikwenda kukagua athari za mafuriko na kuwapa pole wananchi hao Jumatatu, Februari 22, 2016, Waziri Mkuu aliwashukuru wadau wote waliojitolea kuwachangia watu waliopata maafa kutokana na mafuriko hayo.

Wadau waliotoa misaada hiyo ni Benki ya NMB mabati 500, mifuko ya saruji 500, kilo 820 za maharage, kilo 750 za unga wa mahindi na lita 250 za mafuta ya kupikia vyote vikiwa na thamani ya sh. milioni 20/-. Wengine ni Mfuko wa Pensheni wa PPF uliotoa mabati 200 na mifuko ya saruji 200 vyenye thamani ya sh. milioni 6.6/-.

Wengine ni Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF) waliotoa mabati 200 na mifuko ya saruji 160 vyenye thamani ya sh. milioni 4.5/-; Kiwanda cha kusindika nyanya cha RedGold kimetoa mifuko ya saruji 100 na mabati 50 vyenye thamani ya sh. Milioni 3/-; mbunge wa viti maalum kwa tiketi ya CHADEMA, Bi. Susan Chogisasa na wenzake wametoa mabati 150, mifuko 23 ya saruji, kilo 100 za maharage, kilo 50 za chumvi na nguo mbalimbali vyote vikiwa na thamani ya sh. milioni 1.3/-. Madiwani wa Iringa Vijijini walitoa sh. 380,000/-, Wabunge wa Viti Maalum kupitia CCM walitoa vifaa vya sh. Milioni 1.7/-; ofisi ya CCM Mkoa wametoa vifaa vya sh. milioni 6.1/-, Kamanda wa UVCCM Mkoa wa Iringa, Bw. Salim Abri aliipatia Halmashauri ya Wilaya ya Iringa sh. milioni 5/- ili wanunue vyakula vya waliopatwa na maafa.

Naye Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi ambaye pia ni mbunge wa Isimani, Bw. William Lukuvi alitoa fedha taslim sh. milioni 20/- kati ya hizo sh. milioni 15 zikiwa ni zake na milioni 5/- ni za Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais - TAMISEMI, Bw. George Simbachawene. Pia alikabidhi seti 251 za mashuka zenye thamani ya sh. milioni 4/- zikiwa ni mchango kutoka Benki ya CRDB. Waziri Lukuvi ambaye alishatoa mabati 250, aliahidi kuongeza mabati mengine 250 (yote yana thamani ya sh. milioni 8), pia alikabidhi sh. milioni 1.5/- kwa diwani wa Mlenge ili ziwasaidie kukodi gari la kukarabati barabara yao ambayo imeharibika sana kutokana na mafuriko hayo.

Mapema, akitoa taarifa ya maafa kwa Waziri Mkuu, Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Bi. Amina Masenza alisema jumla ya kaya 82 zilikosa makazi kutokana na mvua zilizonyesha Februari 12 na kusababisha mafuriko. Kabla ya hapo, kaya nyingine 75 zenye wakazi 377ziliathirika kutokana na mvua zilizoanza Februari 3, mwaka huu. Alisema miundombinu ya barabara na ya maji safi iliharibiwa vibaya na kusababisha hasara ya zaidi ya sh, milioni 250/-. Pia wakazi hao walikubwa na uginjwa wa kipindupindu kutokana na mto Mapogoro kufurika na kusomba baadhi ya vyoo vya wakazi hao. “Tangu Februari mosi, wamekwishapokea waginjwa wa kipindupinda 351 llakini walioko wodini hivi sasa ni wagonjwa 25 tu,“ alisema Mkuu huyo wa mkoa.

Na Ofisi ya Waziri mkuu.








All the contents on this site are copyrighted ©.