2016-02-23 09:45:00

Wasi wasi kuhusiana na Mkataba Mtambuka wa Bahari ya Pacific


Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Amerika ya Kusini, CELAM, linaonesha wasi wasi mkubwa kutokana na Mkataba Mtambuka wa Bahari ya Pacific uliotiwa sahihi hivi karibuni na nchi kadhaa za Amerika ya Kusini, baadhi yao zimeonesha utashi wa kisiasa wa kutaka kuridhia mkataba huu, ingawa China haijaridhia bado. Huu ni mkataba unaounda sheria na kanuni zinazoratibu uchumi mamboleo: kuhusiana na takwimu za kimataifa pamoja na changamoto ya mashirika na makampuni ya kitaifa na kimataifa kuwa na ushindani katika mchakato wa uzalishaji na utoaji huduma.

Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Amerika ya Kusini, CELAM, linaonesha wasi wasi mkubwa kuhusiana na madhara ya mkataba huu katika sekta ya afya, kwani kuna uwezekano mkubwa wa makampuni ya dawa kuwa na umiliki wa utengenezaji na usambazaji wa dawa, hali ambayo inaweza kuhatarisha ubora wa maisha ya mamillioni ya watu huko Amerika ya Kusini. Kanisa kwa kuwa na mwono mpana na sauti ya kinabii, linawataka wadau mbali mbali wa sekta ya uchumi kutoa kipaumbele cha kwanza kwa utu na heshima ya binadamu.

Watu wapate dawa muhimu kwa kadiri ya uwezo wao, vinginevyo, maskini na akina “yakhe pangu pakavu tia mchuzi” wataishia pabaya! Mkataba mtambuka wa Bahari ya Pacific ulete mafao kwa wananchi badala ya kutafuta faida kubwa kwa gharama ya maisha ya maskini huko Amerika ya Kusini. Wadau mbali mbali waendeleze mchakato wa majadiliano kwa binadamu kupewa kipaumbele cha kwanza kuliko faida kubwa za kiuchumi.

Kutokana na wasi wasi huu, Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Amerika ya Kusini linapania kupeleka kesi hii kwenye Tume ya haki za binadamu Amerika ya Kusini katika mkutano wake unaotarajiwa kufanyika hapo tarehe 4-8 Aprili 2016. Tamko hili la Maaskofu wa CELAM limetolewa baada ya kuhitimisha semina ya kimataifa iliyokuwa inachambua changamoto za Baba Mtakatifu Francisko anayelitaka Kanisa kutoka ufichoni, tayari kuwatangazia watu wa mataifa Injili ya furaha kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa maskini kwa ajili ya maskini; tema inayovaliwa njuga kwa sasa na Baba Mtakatifu Francisko kwa kutambua kwamba maskini ni kiini cha Habari Njema ya Wokovu. Semina hii imefanyika hivi karibuni hiko Bogotà, Colombia.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.