Baba Mtakatifu , Jumanne akihubiri katika Kanisa ndogo la Mtakatifu Marta, ndani ya Vatican , amesema Ukristo ni kutenda mema na si porojo za kinafiki na ubatili. Pia ameasa kwamba, wakati huu wa Kwaresima, hutukumbusha njia inayofaa kutembea katika maisha .
Homilia Baba Mtakatifu Francisko, imekemea tabia ya unafiki, kujionyesha kwa maneno kama ni mtu wa dini, lakini kumbe kimatendo ni mbali na dini. Aliendelea kuyazungumzia maisha thabiti ya Mkristo, kwamba humwonyesha Mungu wa kweli. Na akaonya Wakristo wanaoishi kinyume na maisha hayo, ambao kinafiki hujionyesha kama ni Wakristo safi lakini kumbe kimaisha utendaji wao uko mbali na Ukristo. Ametaja unafiki huo hulidhoofisha kanisa, kwa kuwa, wasio Wakristo hawezi ona ukweli wa Ukristo na hivyo hujiweka mbali. Aliendelea kueleza juu ya Wakristo wanafiki ambao hutenda kwa ufahali na majivuno ya maneno badala ya kutenda kwa unyenyekevu, kuwajali wahitaji na maskini zaidi.
Tafakari ya Papa , ililenga kufafanua aya za Liturujia ya Neno la Siku, ambamo nabii Isaya na Injili ya Mathayo, kwa mara nyingine wanaeleza kinachotakiwa kufanywa na muumini Mkristo. Papa Francisko alikazia zaidi maneno ya Yesu, ambamo ameuzungumizia unafiki wa Waandishi na Mafarisayo,na kuwataka wanafunzi wake na umati wa watu waliokuwa wakimsikiliza, kuyachukua yale wanayofundisha walimu hao na si kuiga matendo yao.
Papa alieleza na kutaja uzoefu wake akisema ni mara ngapi tunasikia mtu akijigamba kuwa Mkatoliki safi , lakini hata hajua kwa wakati huo Kanisa liko ktiak kipindi gani na linafanya nini , au mara ngapi wazazi husema wao ni Katoliki lakini hawana hata muda wa kuzungumza na watoto wao juu ya maisha ya Mkatoliki yanavyo paswa kuwa. Aidha alitoa mfano wa watu wanaopeleka wazazi wao katika nyumba za wazee na kuwatelekeza huko, badala ya kuishi nao.
Papa mara kwa mara pia alirejea maneno ya Isaya, yenye kuonyesha kile Mungu anachotaka kwa biandamu kwamba hasa ni kuachana na matendo maovu, badala yake ajifunze kuw amtu mwema . Ni kuacha na dhuluma na kutenda kwa haki . Ni kutetea yatima na wajane wanaonewa na si kuwagandamiza. Ni kuwaonyesha wengine huruma ya Mungu isiyokuwa na mwisho kwa binadamu, Mungu anayetoa mwaliko daima wa kuingia katika mazungumzo nao hata kwa mwenye dhambi nyingi, yeyé atazitakasa na kuzifanya kuwa nyeupe kama heluji .
Hiyo ndiyo huruma ya Mungu ambayo hutolewa kwa wale wanaopenda kukutana naye katika majadiliano ya kweli , kuhusu mambo ya kufanya na yale yasiyofaa . Huu ni upendo mkubwa wa Bwana kati ya kusema na kutenda. Kuwa Mkristo ina maana ya kutenda. Kufanya mapenzi ya Mungu kila siku hadi siku ya mwisho, ambapo Bwana atarejea na kuuliza ulifanya nini kwa ajili yangu?
Baba Mtakatifu alikamilisha homilii ayake kwa kuomba hekima za Bwana, zituwezeshe kuelewa tofauti kati ya kusema na kutenda , zitufundishe njia ya kufanya na kutusaidia kutembea katika barabara ya wema na huruma kimatendo , kwa sababu barabara ya maneno bila vitendo ni sawa na barabara waliyotembea walimu wa sheria na Mafarisayo waliotajwa katiak Injili , ambao walipenda kuhutubia watu kwa maneno , lakini utendaji wao ukiwa mbali na hayo waliyoyahubiri. Amemwoba Bwana atufundishe njia ya Injili.
All the contents on this site are copyrighted ©. |