2016-02-23 07:34:00

Matendo ya huruma yanapaswa kumwilishwa katika huduma!


Siku kuu ya Ukulu wa Mtakatifu Petro inayoadhimishwa na Mama Kanisa kila mwaka ifikapo tarehe 22 Februari kwa mwaka 2016 imechukua mwelekeo tofauti kabisa, kwa Baba Mtakatifu Francisko kuungana na wafanyakazi wote wa Vatican katika maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu. Maadhimisho haya yameanza kwa tafakari ya kina iliyotolewa na Padre Marko Ivan Rupnik na kuhudhuriwa na Baba Mtakatifu na hatimaye, akashiriki pia katika maandamano kuelekea kwenye Lango la huruma ya Mungu, Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican.Baba Mtakatifu Francisko katika mahubiri yake, amewataka wafanyakazi wa Vatican kutambua kwamba, hii ni Jumuiya ya huduma kwa familia ya Mungu, dhamana inayopaswa kutekelezwa kwa uaminifu, huruma na kwamba, asiwepo mtu anayejisikia kutothaminiwa au  kudharauliwa!

Padre Rupnik katika tafakari yake iliyohudhuriwa na umati mkubwa wa wafanyakazi wa Vatican kwenye Ukumbi wa Paulo VI amekazia umuhimu wa wafanyakazi wa Vatican kuwa huru, kujitoa bila ya kujibakiza na kuonesha moyo wa ukarimu na mapendo. Hizi ni sifa ambazo mfanyakazi wa Vatican anapaswa kuzimwilisha katika maisha na utume wake kwa kutambua kwamba, binadamu katika ulimwengu mamboleo anakumbana na changamoto na matatizo mengi yanayomwachia madonda katika maisha yake.

Kwa kutambua hali hii, wafanyakazi wa Vatican wanapaswa kuhakikisha kwamba, wanamwilisha matendo ya huruma katika maisha na utume wao, ili kuwapatia watu wa Mungu fursa ya kuanza tena upya! Ili kweli ushauri wa Kanisa uweze kuwa na mvuto katika maisha ya kijamii, kuna haja ya kuonesha ujumbe huu katika ushuhuda wa maisha unaojikita katika uongozi bora, miundo mbinu inayowajibika barabara bila kuwabagua watu kwa kuonesha hali halisi; ili kuamsha kiu ya watu kutaka kupyaisha maisha yao, chachu inayobubujika kutoka kwa Kristo na Kanisa lake.

Kanisa liwe ni Sakramenti ya Umoja wa Fumbo la Utatu Mtakatifu na huruma ya Mungu inayomwilishwa katika maisha na utume wa Kanisa kwa watu wa nyakati hizi. Kwa mantiki hii, binadamu anakuwa ni mahali ambapo umoja unamwilishwa kama ilivyo kwa huruma katika Kanisa. Maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu kwa wafanyakazi wa Vatican ni muda muafaka wa kufanya tafakari ya kina ili kuondokana na vishawishi vya malimwengu na ubinafsi na badala yake kuambata umoja na mshikamano kama sehemu ya viungo hai vya Fumbo la Mwili wa Kristo yaani Kanisa.

Padre Rupnik anakaza kusema, Kanisa linaweza kusaidia kuleta mchakato wa mageuzi na mabadiliko katika jamii kwa kujikita katika umoja mintarafu Fumbo la Utatu Mtakatifu. Kwa kuonesha na kushuhudia uso wa Mwana wa Mungu; kwa kuendelea kujiandaa kwa ujio wake sanjari na kuendeleza kazi ya ukombozi kwa mwanadamu anayeogelea katika dimbwi la dhambi na mauti. Hatua ya pili ni kutambua uwepo endelevu wa Roho Mtakatifu anayeliwezesha Kanisa kudumisha kipaji cha ugunduzi mintarafu Ufunuo wa Mungu unaoambata upendo unaowashirikisha wote. Viongozi wa Kanisa wanapaswa kutekeleza wajibu wao kikamilifu ili kuonesha na kushuhudia kazi ya Mungu inayotekelezwa katika maisha ya binadamu kwa njia ya huruma, kielelezo cha mshikamano unaowashirikisha wote.

Padre Rupnik anakaza kusema, ujio wa Kristo umeliwezesha Kanisa kuwa na mwelekeo mpya wa maisha na utume wake. Ukristo si dini inayojikita zaidi katika mafundisho tanzu, Mapokeo, Sheria na Kanuni ambazo mwamini anapaswa kuzitekeleza ili aweze kupata neema na baraka kutoka kwa Mungu. Kristo Yesu ni ushuhuda wa dini inayompatia mwanadamu kipaumbele cha kwanza na kwamba, sheria na kanuni ni kwa ajili ya binadamu na wala si binadamu kwa ajili ya sheria. Upendo uwe ni kiini cha maisha ya Kikristo yanayojikita katika huduma.

Mwenyezi Mungu anampatia mtunza shamba la mizabibu dhamana ya kuendeleza kazi yake, hapa lengo si mzabibu, bali divai itakayotumika kumrudishia mwanadamu furaha ya ndani kama ilivyokuwa kwenye Arusi ya Kana ya Galilaya. Binadamu anapaswa kushikamana na Muumba wake, ili kutekeleza mpango wa Mungu katika maisha yake, vinginevyo, kifo kitakuwa ni mchungaji wake wa daima. Padre Marko Ivan Rupnik anahitimisha tafakari yake katika maadhimisho ya Siku kuu ya Ukulu wa Mtakatifu Petro, sanjari na Maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu kwa wafanyakazi wa Vatican kwa kusema kwamba, ikiwa kama mwamini atafanikiwa kuruhusu maisha ya Mungu yapitie ndani mwake, hapo ataweza kuzaa matunda na kazi zake kuendelea kudumu kwani yote haya yanarejea tena kwa Mwenyezi Mungu mwingi wa huruma na mapendo!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

 

 








All the contents on this site are copyrighted ©.