2016-02-23 07:53:00

Afrika ya Kati inataka kuandika ukurasa mpya!


Wananchi wa Jamhuri ya watu wa Afrika ya Kati wamemchagua Bwana Faustin-Archange Touadèra kuwa Rais wao baada ya kujinyakulia asilimia 62.71% ya kura zote halali zilizopigwa katika uchaguzi mkuu wa marudio uliofanyika hivi karibuni na hivyo kumbwaga mpinzani wake Anicet- Georges Dologuèlè aliyejipatia asilimia 37.29% ya kura zote halali zilizopigwa. Taarifa hizi zimetolewa na vyombo vya habari nchini Jamhuri ya Watu wa Afrika ya Kati vikimnukulu Marie Madelein Nkouet msimamizi mkuu wa uchaguzi nchini humo.

Wachunguzi wa mambo wanasema Touadèra aliwahi kuwa Waziri mkuu katika jamhuri ya Watu wa Afrika ya Kati kuanzia mwaka 2008 hadi mwaka 2013 atakuwa na changamoto kubwa mbele yake katika mchakato wa kuirejesha tena Afrika ya Kati katika misingi ya haki, amani, maridhiano na umoja wa kitaifa baada ya mipasuko ya: kidini, kisiasa na kijamii kujitokeza nchini humo na kupelekea vita na machafuko yaliyosababisha maafa makubwa kwa watu na mali zao.

Haya yalikuwa ni mapambano yaliyofunikwa kwa pazia la udini kati ya Seleka na Balaka, lakini wachunguzi wa mambo wanasema, kinzani hizi za kidini zilitumiwa na baadhi ya wanasiasa waliotaka kujiimarisha kisiasa kwa kutumia udini. Ushindi wa Bwana Touadèra unaonesha kiu ya wananchi wa Afrika ya Kati ya kutaka kufanya mageuzi na kuanza kuandika ukurasa mpya baada ya machafuko yaliyotokea kunako mwaka 2013. Bwana Faustin-Archange Touadèra anachukua nafasi ya Bibi Catherine Samba-Panza aliyeteuliwa kuwa ni Rais wa kipindi cha mpito nchini Afrika ya Kati.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

 

 








All the contents on this site are copyrighted ©.