2016-02-22 14:28:00

Wakristo wameathirika vibaya sana kutokana na vita huko Mashariki ya Kati!


Vita na machafuko ya kisiasa huko Mashariki ya Kati yamekuwa na athari kubwa katika maisha, utamaduni na mapokeo ya wananchi wa eneo hili, kiasi kwamba Wakristo waliokuwa wanaishi katika eneo hili wanalazimika kuyahama makazi yao kutokana na chuki za kidini na mashambulizi yanayofanywa na waamini wenye misimamo mikali ya kidini, kiasi hata cha kuhatarisha mshikamano na mafungamano ya kijamii. Wakristo wanauwawa na kuteseka huko Mashariki ya Kati kutokana na imani yao kwa Kristo na Kanisa lake!

Haya yamesemwa hivi karibuni na Kardinali Fernando Filoni, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa watu, wakati alipokuwa anashiriki katika mkutano wa elimu kwenye Chuo kikuu cha Kitaifa cha Budapest, Hungaria kuhusiana na athari za kidini mintarafu wimbi kubwa la wahamiaji linalotafuta usalama na hifadhi kwenye nchi za Ulaya. Kardinali Filoni akizingumzia kuhusu Kanisa nchini Iraq, amegusia historia, maendeleo na utume wake tangu mwanzo hadi nyakati hizi. Kardinali Filoni pia ameandika kitabu kuhusiana na mchango wa Kanisa huko Iraq, kitabu ambacho kwa sasa kinatafsiriwa katika lugha ya Kiarabu, Kiingereza na Kihispania.

Kanisa limekuwepo huko Iraq kwa takribani miaka elfu mbili iliyopita na wengi wa Wakristo walikuwa wakiishi katika eneo ambalo lilikuwa linajulikana kama Mesoptamia. Wakati huo, idadi ya Wakristo ilikuwa si chini ya asilimia 15% ya idadi ya wananchi wote wa Mesoptamia, lakini leo hii kutokana na vita, chuki za kidini na mipasuko ya kijamii, idadi ya Wakristo imebaki chini ya asilimia 2% ya idadi ya wananchi wote wa Iraq. Zaidi ya waamini millioni 1. 2 waliuwawa kikatili kutokana na chuki za kidini, ubaguzi na ukosefu wa maridhiano kati ya wananchi.

Kardinali Fernando Filoni anafafanua kwamba kunako mwaka 2014 alitumwa na Baba Mtakatifu Francisko kwenda Mashariki ya Kati ili kuwaonesha wananchi wa eneo hili mshikamano wa Kanisa katika shida na mahangaiko yao. Kuna mambo makuu matatu yanayowaunganisha wananchi wa Bara la Ulaya: dini inayojikita katika maisha ya watu; uzuri na sanaa pamoja na haki. Ukosefu wa misingi ya haki na amani huko Mashariki ya Kati kumepelekea makundi makubwa ya wahamiaji na wakimbizi, ambayo kwa sasa yanaonekana kuwa ni kero na usumbufu mkubwa kwa Umoja wa Ulaya. Kila mtu ana haki ya kuishi katika mazingira ya amani. Ikumbukwe kwamba, dhana ya uhamiaji wa makundi makubwa ya watu chanzo chake ni vita, kinzani na mipasuko ya kidini, kisiasa na kijamii!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.