Kwa ajili ya kipindi hiki cha Kwaresima,Jumapili wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana, Baba Mtakatifu Francisko alitoa kiboksi kidogo cha zawadi , kilichotajwa ndani mwake kuwa na dawa ya kiroho ya Huruma ya Mungu. Dawa hiyo ni Rosare ndogo na Sanamu ya Huruma ya Yesu.
Katika hotuba yake, alikumbusha maana ya kipindi cha kwaresima akisema huu ni wakati kukamilisha safari ya uongofu , ambayo kiini chake ni matendo ya huruma, yenye kuonyesha huruma ya Mungu. Na alimtaka kila mwamini kuipokea zawahi hii kama msaada wake wa kiroho, na hasa katika wakati huu wa Mwaka wa Huruma, waweze kueneza upendo, msamaha, na udugu kati ya Watu.
Hii ilikuwa ni mara ya pili kwa Papa kutoa ishara ya "zawadi ya Huruma ya Mungu" kwa waamini. Mara ya kwanza alifanya hivyo, Novemba ya 2013, wakati wa kukamilika wa Maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Imani , ambamo aliwataka waamini kutumia "dawa hiyo ya kiroho" kwa ajili ya kuzaa matunda yaliyo thabiti zaidi ya kiroho kutokana na neema walizozipata wakti wa maadhimisho ya mwaka wa Imani . Katika matukio yote mawili, zawadi hii ya Papa , ilisambazwa na wafanyakazi wa kujitolea, kwa watu wote bila kujali hadhi yao , wakiwemo pia watu maskini wasio na makazi, wakimbizi, na maskini wahamiaji.
Papa: awataka Wakristo kukomesha adhabu ya kifo
Aidha Jumapili iliyopita, Papa alitoa wito kwa Wakristo na watu wote wenye mapenzi mema ,kutenda kwa ushupavu zaidi, kwa ajili ya kuhakikisha adhabu ya kifo inafutwa katika uso wa dunia, na hali ya maisha namzingira katika magereza, vinaboreshwa, kwa kuwa kufungwa hakupotezi heshima ya utu wa mtu. Baba Mtakatifu Francisko alitoa rai hiyo, baada ya sala ya Malaika wa Bwana.
Wito wa Papa ulilenga hasa kuwataka viongozi wa serikali,waridhie utiaji wa saini katika hati ya makubaliano ya kimataifa, inayotaka kufutwa kwa adhabu ya kifo duniani. Na ombi lake liliwalenga Viongozi Wakatoliki, akiwataka wawe na ujasiri wa kuwa mfano katika kukataa kutekeleza hukumu yoyote ya kifo, na hasa katika mwaka huu Mtakatifu wa Huruma ya Mungu. Papa alitoa ombi lake akiangalisha katika mazingira ya uwepo wa Kongamano la Kimataifa kwa ajili ya kukomesha adhabu ya kifo, Jumatatu hii, kama inavyo hamasishwa na Jumuiya ya Mtakatifu Egidio, chini ya Kaulimbiu” Dunia isiyokuwa na adhabu ya kifo."
Baba Mtakatifu ameonyesha matumaini yake kwamba, kongamano hili, litaweza kutoa msukumo mpya katika juhudi zinazolenga kukomesha adhabu ya kifo, juhudi zinazoonekana kupambana na upinzani zaidi ,hata katika vyombo halali vya ulinzi jamii. Amesema, jumuia za kisiasa na kijamii, zina njia nyingi zinazoweza kupambana na uhalifu bila kumpokonya mhalifu haki yake ya kujirekebisha na kuongoka. Papa aliiweka hoja hii ya adhabu ya kifo katika mtazamo wa mfumo wa mazingira ya kisheria yenye kwenda sambamba na heshima ya mwanadamu katika mpango wa Mungu wa wokovu. Alifanya rejea katika Maandiko Matakatifu, “Amri, 'Usiue', akisema kuwa amri hiyo ni ya thamani sana, na huwalenga watu wote, wenye hatia na wasio na , kwamba, kwao wote wana haki isiyoweza ondoshwa kwao , haki ya kuishi , kama zawadi ya Mungu.
All the contents on this site are copyrighted ©. |