2016-02-20 16:15:00

Tambueni utashi na utukufu wa Mungu


Katika somo letu la kwanza tunaona kuwa Mungu alipomwita Abrahamu toka nchi ya Baba zake, alimwahidi jina kubwa na uzao mkubwa. Wito huu wa Abrahamu ulifanyika katika sura ya  12:1-3. Sasa baada ya miaka kadhaa bado hana cho chote, yaani hana jina wala uzao, lakini bado anamwamini Mungu. Hapa tena nafasi ya Mungu inaonekana. Mungu hasahau ahadi aliyotoa. Daima Mungu anachukua jukumu kama ulivyo upendo wake – anaingilia kati. Na anapoingilia kati huwa anatoa wokovu na hapa kwa njia ya ahadi.

Katika sura ya hii ya 15 ya kitabu cha Mwanzo tunaona jinsi Mungu anavyorudia ahadi yake kwa Abrahamu. Ila Abrahamu hana mrithi wala jina bado, hivyo anataka uhakika fulani ili kuonesha kuwa ahadi hizo zitatokea kweli. Mungu anamwonesha hilo kupitia ibada ya kuchoma wanyama. Kinachoonekana hapa na kuhitajika, kwa Abrahamu na kwetu (wakristo) ni imani kuwa Mungu hutimiza ahadi zake. Nabii Yer. 34:18 - anaonesha haja ya kuheshimu kiapo na kuwa waaminifu katika maagano yao, kushindwa kufanya hivyo tutagawanywa vipande vipande kama wale wanyama. Jamii mbalimbali za kiafrika hutimiza ahadi zao kwa maagano. Wako hata tayari kujitakia kila aina ya balaa iwapo hawatatimiza hayo – Za. 7:3-5, 137:5-6. Kwa kifupi katika sura hii tunaona ahadi na agano.

Hata katika hali hii ya wasiwasi, Abrahamu anaendelea kuamini katika Mungu ambalo ndilo jibu la kwanza na kinachotegemewa toka kwa mwanadamu. Mwitiko huu unabeba kukubali, kujitoa kwa Mungu anayeahidi na hapa imani kuu yahitajika. Katika Gal. 3:6-9 na Rom. 4:1-25, Mt. Paulo daima katika maisha yake aliishangaa imani hii kuu, ya namna hii ya Abrahamu. 

Wanyama kukatwa vipande viwili, kwaonesha kugawanyika kwetu ikiwa tutakiuka ukubali huo. Kule kupita katikati ya vipande vya wanyama, kwaonesha ukubali na kuratibisha agano. Hapa tunaona kama kawaida, Mungu anajiweka katika mstari wa wokovu. Anatuokoa, tukiitikia. Hilo giza kuu, lengo ni kuonesha Mungu anataka kufanya jambo kubwa kwa watu wake. Mungu anakuja kwetu. Ni vigumu kwetu kuelewa jambo hili ingawa twatakiwa kusema mapenzi yako yatimie hata katika wasiwasi na hofu zilizo mbele yetu – Ayu. 4:13-14.

Katika somo la pili twaona jinsi Mt. Paulo anavyokazia umuhimu wa hali ijayo kwa wale wanaomwamini Kristo. Paulo hasiti kusema niigeni mimi kwa vile yeye amemwiga Kristo ipasavyo. Anatualika kukumbuka kuwa sisi ni raia wa mbinguni. Anasisitiza juu ya haki ya kweli na hamu ya kuwa na Kristo. Huu ni mwaliko wa kuwa na imani thabiti huku tukitumainia ukamilfu wa mapenzi ya Mungu.

Katika somo la injili tunaona na kusikia juu ya utukufu wa Mungu – Yesu anageuka sura. Baada ya kuwaeleza juu ya kujikana na kuchukua msalaba, anageuka sura. Ni ajabu kidogo kwani Yesu anaonesha kuushinda ulimwengu kwa kufa msalabani. Anageuka sura baada ya kuwaeleza masharti juu ya ufuasi – lazima kujikana, kuchukua msalaba na ikiwa hivyo basi uhakika wa kufika mbinguni unawekwa wazi.

Somo la injili la leo latupa changamoto kubwa pia. Kina Petro wanashikwa na mshangao mkubwa, hawakuelewa. Mungu anaonesha utukufu wake, ila mwanadamu anashindwa kuulewa. Wao walilala usingizi, ila sauti ya Mungu inasikika. Kile kile kilichotokea wakati wa ubatizo wake Bwana – Lk. 3:22, ndicho kinajirudia tena hapa. Mungu anamweka wazi Yesu hadharani. Hapa imani yetu inaguswa tena leo. Ni kwa jinsi gani tunasikia sauti ya Mungu. Je tuko macho au usingizini? Je sura zetu zikoje? Je kipindi hiki cha Kwaresima sura zetu zitageuka?

Mtume Paulo – Efe. 3:14-21 – anazungumzia uwepo wa mwaliko, uwezo wa kufahamu na kupenda fumbo hilo la Mungu ili kwaresima hii izae matunda na hatimaye tuufikie uzima wa milele katika ufufuko na Kristo. Yaani Pasaka ya mbinguni. Kwa sababu ya kukosa imani, Mtume Paulo analia juu ya maadui wa msalaba – wanaong’ang’ania mambo yao na mambo ya dunia.

Mtume Paulo anataja sana fadhila za imani, matumaini na mapendo ingawa katika mfululizo tofauti. Paulo anasisitiza imani bila matendo ni bure na hakuna wokovu – Rum. 1:16 – Kristo amekufa bure kama mmoja angejiokoa kwa matendo yake mwenyewe. Baada ya kupata uaadilifu kwa imani ya Kristo, imani hiyo ni lazima izae matendo mema ya mapendo – 1Thes:1:3, Gal. 5:6. Ndiyo sababu kila mmoja atahakumiwa kwa kadiri ya matendo hayo ya mapendo – Rum. 2:6.

Tumsifu Yesu Kristo,

Pd. Reginald Mrosso, C.PP.S.








All the contents on this site are copyrighted ©.