2016-02-19 08:18:00

Rais wa Marekani kutembelea Cuba baada ya miaka 90!


Rais Barack Obama wa Marekani anatarajiwa kufanya safari ya kiserikali nchini Cuba kuanzia tarehe 21 hadi tarehe 22 februari 2016. Tukio hili linafanyika baada ya miaka 50 ya kutunishiana misuli kati ya Marekani na Cuba na miaka 90 tangu Rais wa kwanza wa Marekani alipotembelea Cuba. Wachunguzi wa mambo wanaona mwelekeo mpya wa majadiliano kati ya nchi hizi mbili yanayopania kujenga utamaduni na madaraja ya watu kukutana.

Itakumbukwa kwamba, nchi hizi mbili kunako mwaka 2014 zilirejesha mahusiano ya kidiplomasia baada ya Rais Obama na Raul Castro wa Cuba kukutana na kuzungumza ana kwa ana wakati wa maziko ya Rais Nelson Mandela wa Afrika ya Kusini, kunako mwaka 2013. Viongozi hawa wawili wakakutana tena kwa mara ya pili tarehe 11 Aprili 2015 wakati wa mkutano mkuu wa Nchi za Amerika huko Panama. Mahusiano ya kidiplomasia kati ya Cuba na Marekani yalivunjika kunako mwaka 1963 wakati Rais Fidel Castro wa Cuba alipoingia madarakani na Marekani ikamwekea vikwazo vya uchumi ambayo vimekuwa na madhara makubwa kwa ustawi na maendeleo ya wengi nchini Cuba.

Cuba inaendelea kuwavutia wawekezaji kutoka Marekani na kwamba, kwa sasa kuna usafiri wa ndege kutoka Havana, Cuba moja kwa moja hadi nchini Marekani. Rais Obama anasema, anapenda kujenga na kudumisha utamaduni wa majadiliano unaopania pamoja na mambo mengine kukuza na kudumisha uhuru wa watu kujieleza kadiri ya sheria za nchi. Rais wa mwisho kabisa kutembelea Cuba alikuwa ni Rais Clavin Coolidge, kunako mwezi Januari 1928 na kupokelewa na Rais wa Cuba wakati huo, Gerardo Machado. Rais Mstaafu Jimmy Carter alitembelea Cuba kunako mwaka 2002 kwa mwaliko binafsi wa Rais Fidel Castro wa Cuba wakati huo!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

 

 








All the contents on this site are copyrighted ©.