2016-02-19 09:12:00

Kardinali Sandri atembelea Cyprus


Hivi karibuni Kardinali Leonardo Sandri, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Makanisa ya Mashariki ameongoza ujumbe wa watu watatu kutoka katika Baraza lake ili kutembelea Cyprus, ambako huko amekutana na kuzungumza na viongozi wa Serikali na Kanisa. Pamoja na mambo mengine, wamejadili hali na misaada ya kibinadamu inayohitajika nchini humo pamoja na huduma kwa wananchi kutoka Cyprus wanaoishi huko Uingereza, Australia, Marekani, Canada na Afrika ya Kusini. Wameangalia kwa pamoja hali tete ya baadhi ya watu kutoweka katika mazingira ya kutatanisha kwa takribani miaka  40 iliyopita.

Taarifa zinaonesha kwamba, kuna zaidi ya Makanisa 500 ambayo yameharibiwa vibaya au kupangiwa shughuli nyingine au kutaifishwa na Serikali. Rais Nicol Anastasiades wa Cyprus alipata nafasi ya kukutana na ujumbe huu na kupongeza juhhudi zinazofanywa na Vatican katika mchakato wa kutaka kukuza na kudumisha misingi ya haki, amani na maridhiano katika Jumuiya ya Kimataifa, lakini zaidi huko Mashariki ya kati. Cyprus nayo ina changamoto zake mintarafu utengano ambao umedumu kwa takribani miaka 42 na kwamba, umefika wakati kwa Cyprus kuanza mchakato wa ujenzi wa umoja wa kitaifa. Cyprus inaishukuru Jumuiya ya Kimataifa kwa kuchangia katika gharama ya kuwahudumia wakimbizi na wahamiaji kutoka Syria, licha ya kupambana na hali ngumu ya uchumi inayoendelea kuisakama Cyprus kwa wakati huu.

Kwa upande wake, Kardinali Sandri amewasilisha salam na matashi mema kutoka kwa Baba Mtakatifu Francisko kwa viongozi wa kidini na Serikali nchini Cyprus. Amesali na kuadhimisha Ibada za Misa takatifu na Wakleri pamoja na watawa nchini humo na kushuhudia kazi na utume unaotekelezwa na watawa wa mashirika mbali mbali nchini Cyprus. Akizungumza na viongozi wakuu wa Kanisa nchini Cyprus, wote wameonesha umuhimu wa kujikita katika mchakato wa upatanisho wa kimataifa ili kweli haki, amani na maridhiano yaweze kutawala akili na mioyo ya watu. Wamepongeza pia juhudi zilizooneshwa kati ya Baba Mtakatifu Francisko na Patriaki Kirill wa Moscow na Russia nzima kwa kukutana na hatimaye, kutoa Tamko la kichungaji, mwanzo wa ushirikiano kati ya Makanisa haya mawili.

Kardinali Sandri na ujumbe wake, wametembelea vijiji kadhaa nchini Cyprus; wamekutana na kuzungumza na wazee na kushuhudia imani yao inayomwilishwa katika maisha ya kila siku. Ametembelea Kanisa la Mtakatifu Gregori, Lango la Huruma ya Mungu, wakati huu wa maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu. Amekutana na wanafunzi na badaye waliweza pia kusali Sala ya Kanisa pamoja na viongozi wakuu wa Kanisa nchini Cyprus. Itakumbukwa kwamba, Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto XVI alitembelea nchini Cyprus kunako mwaka 2010.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.